Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya imefika katika Shule Shikizi ya Isyesye iliyopo kata ya Igale kutolea ufafanuzi video inayosambaa ikionyesha wananchi wa Kitongoji cha Isyesye,wakilalamikia shule yao Shikizi kutosajiliwa licha ya kuwepo kwa miaka 12 sasa.
Halmashauri hiyo chini ya Mkurugenzi wake Erica Yegella imefika shuleni hapo na kutoa ufafanuzi wa video hiyo kwa wananchi.
Akizungumza Machi 10,2025 Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri mtendaji wa Halmashauri hiyo Afisa Elimu wa Wilaya hiyo anayeshughulikia Elimu ya Msingi Mwalimu Tanu Kameka pamoja na maafisa wengine walifika eneo kilipo Kituo hicho kujionea uhalisia wa hoja za wananchi kisha kufanya Mkutano wa hadhara.
Akitoa ufafanuzi zaidi Afisa Elimu halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Mwalimu Tanu Kameka amesema uwepo wa shule hiyo shikizi eneo lao ipo kihalali na ili isajiliwe vipo vigezo vinavyotakiwa kufuatwa huku akiwaonesha Mdhibiti Ubora wa Wilaya hiyo Mary Makali.
Akizungumza kijijini hapo Mwalimu anayejitolea kuwafundisha wanafunzi wa Kituo hicho Shikizi cha Isyesye,Gwakisa Adamson pamoja na baadhi ya wanafunzi waliokuwepo shuleni hapo na wananchi wenyewe walikiri ukweli ulioonekana na kwamba katika hoja za ndani ya video iliyosambaa walitamka ikiwa ni kutaka kusikika ukubwa wa hitaji lao.
Akiwasomea vigezo vinavyotakiwa shule Shikizi kusajiliwa na kuwa Shule ya Msingi, Mary Makali amesema
inatakiwa iwe na vyumba vya madarasa 6, Ofisi za walimu 2, matundu ya vyoo vya wanafunzi wa kike 6, wavulana matundu Matano na vyoo vya walimu Matundu Mawili na viwe mbali na vyoo vya wanafunzi.
Makali amewataka wananchi kuendelea kushikamana na kushirikiana na Halmashauri yao wanapotaka kujenga ili kupewa wataalam .
Mmoja wa wananchi waliojitolea ardhi kujenga kituo Shikizi hicho Jumanne Mwasembo amesema wamefurahishwa na ufafanuzi uliotolewa na kwamba awali walikuwa hawafahamu vigezo hivyo.
Shule hiyo Shikizi ya Isyesye ina darasa la awali hadi la 3 na jumla kuna wanafunzi 95,walimu 3 wa kujitolea wawili ambao wamemaliza Kidato cha 4 na mmoja amehitimu mafunzo ya Ualimu grade A.
Kuna madarasa 2 yaliyojengwa na Serikali kupitia COVID Disemba 2022, Boma lenye madarasa 2 limejengwa kwa nguvu za wananchi, vyoo vya kienyeji matundu 4, madawati yapo 55 ya kukaa wanafunzi 3 kwa kila dawati.
Viongozi hao mara baada ya kufanya mkutano wa hadhara kijijini hapo walizunguka eneo la kituo shikizi wakiwa wameongozana na wananchi na kugundua kuwa hoja ya uwepo wa madarasa Matano haikuwa kweli bali yapo Madarasa Mawili yaliyojengwa na Serikali na boma Moja lenye vyumba viwili na ofisi Moja ya walimu.
Hata hivyo lilipochukuliwa daftari la usajili na mahudhuria ya wanafunzi (Attendance) ilibainika uwepo wa Wanafunzi 95 na siyo 128 kama walivyoeleza wananchi hao katika video iliyosambaa mitandaoni na wanafunzi hao wameishia darasa la Tatu na siyo Darasa la Tano kama madai ya awali ya wananchi hao



More Stories
Kapinga azindua namba ya bure ya huduma kwa wateja wa TANESCO
RC.Sinyamule mgeni rasmi Misa wadau summit 2025
Miaka minne ya Rais Samia TRA yaongeza makusanyo ya kodi kwa asilimia 78