Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya (Mbeya DC) imepiga hatua kubwa katika kuimarisha lishe, ikiwemo kupunguza kiwango cha udumavu kutoka asilimia 21 hadi asilimia 18, pamoja na kuboresha huduma za lishe kwa mama wajawazito na watoto katika vituo vya kutolea huduma.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho siku ya lishe duniani yalioanza Novemba 17,2025 na kuhitimishwa Novemba 21
Afisa Lishe wa Halmashauri hiyo,Namkundaelly Mmbaga, amesema mafanikio hayo yametokana na jitihada za kuhimiza lishe bora kwa makundi mbalimbali, hasa watoto na akina mama wajawazito, kupitia programu na kampeni zinazoendelea katika jamii.

“Maadhimisho haya ya mwaka huu ni vema tutumie kuhimiza lishe bora,hususan kwa watoto wadogo na akina mama wajawazito kwani vituo vyetu vya huduma vimekuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya lishe,ni muhimu jamii kuzingatia maelekezo yanayotolewa,” amesema Mmbaga.
Pia ameongeza kuwa watu wazima wanapaswa kubadili mifumo mibaya ya ulaji, ikiwemo matumizi makubwa ya vyakula vyenye sukari nyingi vinavyoweza kusababisha magonjwa nyemelezi.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri hiyo,Emiliana Mbise akimwakilisha Mganga Mkuu wa Halmashauri, amewataka wananchi kuzingatia programu jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto ili kuhakikisha afya bora kuanzia ujauzito hadi utoto.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa mwaka 2025 ni “Afya ni mtaji wako, zingatia unachokula.”Kilele cha maadhimisho hayo kwa Mbeya DC kimefanyika katika Chuo cha Ufundi cha Maendeleo ya Wananchi Nzovwe, kilichopo Kata ya Bonde la Songwe.
Halmashauri ya wilaya hiyo chini ya mkurugenzi wake Erica Yegella imekuwa katika mikakati ya kuhakikisha wilaya hiyo inaondokana na Udumavu na kuweka kipaumbele suala la lishe kwa wananchi.
Mmoja wa wananchi walioshiriki maadhimisho hayo, Tatu Juma amesema jamii imepiga hatua kubwa katika kuzingatia lishe, hasa kwa watoto na wanawake wajawazito.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi