Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mbeya
KUFUATIA mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha Januari 15, 2026 na kuharibu miundombinu katika Shule ya Sekondari Usongwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imeahidi kutoa shilingi milioni 20 kwa ajili ya ukarabati wa mabweni ya wanafunzi wa kike wa kidato cha sita, ofisi moja ya walimu pamoja na chumba kimoja cha zahanati ili shughuli za masomo ziendelee kama kawaida.
Kauli hiyo ilitolewa Januari 27, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegella, wakati akiongoza zoezi la upandaji wa miti zaidi ya 1,350 katika eneo la Shule ya Sekondari Usongwe, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Fedha hizi zitasaidia kukarabati majengo yaliyoharibiwa na mvua iliyonyesha Januari 15 mwaka huu, ambayo ilisababisha uharibifu wa mali mbalimbali ikiwemo nguo za wanafunzi na mahitaji mengine muhimu ya shule,” amesema Yegella.
Kwa upande wake, Afisa Maliasili na Utunzaji wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Gerald Shayo, amesema jumla ya miti 1,350 imepandwa katika Shule ya Sekondari Usongwe ikiwa ni kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amechagua maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa kwa kufanya shughuli za utunzaji wa mazingira.

“Hivyo tumeona ni busara kupanda miti hapa ili wanafunzi wajifunze umuhimu wa utunzaji wa mazingira na kuepusha majanga yanayoweza kutokea baadaye,” amesema Shayo.
Akisoma taarifa ya shule hiyo, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Usongwe, Leonard Chuwa, amesema shule ilikumbwa na madhara makubwa kufuatia mvua iliyoambatana na upepo mkali Januari 15, 2026, hali iliyosababisha kuezuliwa kwa paa la bweni la wanafunzi wa kike wa kidato cha sita, ofisi ya walimu pamoja na jengo la zahanati.
Amesema mvua hiyo, iliyoambatana na upepo mkali unaodaiwa kuhusishwa na kimbunga, ilinyesha majira ya saa nane mchana na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo kuharibika kwa mali za wanafunzi wapatao 50, zikiwemo taulo za kike, madaftari, mashuka, magodoro yaliyolowa maji, jiko la shule pamoja na vifaa vya ofisi za walimu.

Chuwa amesema shule hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wanafunzi na watumishi kuhusu namna ya kukabiliana na majanga ya asili, hususan upepo mkali na kimbunga, huku mkakati mkubwa ukiwa ni kupanda miti kuzunguka eneo la shule ili kupunguza athari za majanga hayo.
“Tunaishukuru sana Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Erica Yegella, kwa hatua za haraka anazochukua pindi majanga yanapotokea. Mwaka jana alitatua changamoto ya kuezuliwa kwa paa la matundu 13 ya vyoo kwa kutoa zaidi ya shilingi milioni tatu,” amesema Chuwa.
Ameongeza kuwa baada ya tukio la Januari 15, 2026, Mkurugenzi Mtendaji huyo alituma wataalamu kwa ajili ya kufanya tathmini ya uharibifu wa majengo na baadaye kuahidi kutoa shilingi milioni 20 kwa ajili ya kurejesha miundombinu iliyoharibika.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina