Na Ester Macha, TimesMajira Online Mbeya
NYOTA wa kikosi cha timu ya Mbeya City wameapa kuwapigisha kwata Maafande wa JKT Tanzania ili kubakiza alama zote tatu nyumbani katika mchezo wao wa leo namba 246 wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) utakaochezwa kwenye uwanja wa Sokoine.
Mbeya City itaingia katika mchezo huo huku ikitaka kuendeleza ushindi na ubabe kwa wapinzani wao ambao walikubali kichapo cha goli 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Novemba 24 katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Timu hizo zitashuka dimbani huku kila mmoja akihitaji alama tatu kwani hadi sasa katika msimamo wa Ligi timu hizo zote zina alama 27 walizopata baada ya wenyeji kucheza mechi 27 na kushinda tano, sare 12 na kupoteza mechi nne huku JKT wakicheza mechi 26 wakishinda saba, sare sita na kupoteza mechi 13.
Kocha mkuu wa Mbeya City, Mathias Lule amesema kuwa, baada ya kufanikiwa kushinda mechi mbili mfululizo katika viwanja vya ugenini, leo wanahamishia nguvu nyumbani kwao hivyo watahakikisha hawafanyi makosa.
Amesema kuwa, ushindi katika mchezo huo ni muhimu sana kwao kwani angalau watakaa katika sehemu salama kidogo kwenye msimamo wa Ligi Kuu ambao sasa hivi wanapambana wasishuke Daraja.
Kocha huyo ameema kuwa, ukiangalia katika ratiba bado wana mechi ambazo ikiwa watafanikiwa na kushinda zote basi watajitoa katika hatari hiyo na kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi ili kuwapa sapoti.
“Tupo nyumbani na mkakati wetu ni kuendeleza ushindi ili kuwapa furaha mashabiki wetu hivyo kama timu tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunapata ushindi ili kuweza kujitoa kwenye nafasi tuliyo sasa na kuwapa furaha mashabiki wetu,” amesema kocha huyo.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025