November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR MAGEUZI, James Mbatia

Mbatia aitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuzingatia haki

Na Doreen Aloyce, TimesMajira Online, Dodoma

MWENYEKITI wa Chama cha NCCR MAGEUZI, James Mbatia ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuzingati haki, sheria, taratibu na kanuni zitakazoongoza uchaguzi utakaofanyika October mwaka huu ili kuwapata washindi katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kudumisha amani na utulivu uliojengeka nchini.

Mbatia ametoa wito huo leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa kikao cha watia nia wa chama hicho katika nafasi mbalimbali za uongozi ambapo amesema kuwa tukio la uchaguzi linazungumzia maisha ya Watanzania katika miaka mingine mitano ijayo na hivyo tukio hilo ni muhimu kufanyika katika hali ya uwazi ili kuepeusha migongano, malalamiko na misuguano ambayo itawagawa Watanzania.

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR MAGEUZI, James Mbatia

“Wale wanaotaka kuwaharibia wakae pembeni kwa sababu wewe mkurugenzi mmoja unaweza kuharibu uchaguzi na kuharibu sifa nzima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutozingatia utaratibu uliowekwa na mamlaka husika,” amesema Mbatia

Mbatia amesema kuwa wananchi wanahitaji kupata viongozi watakaosaidia kusukuma mbele jitihada ambazo tayari zimefanywa na serikali na hivyo wananchi wanataka kuona maendeleo karibu katika kila nyanja wakiwemo vijana kupata ajira, waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa weledi wakiwa na vifaa vya kisasa hivyo ni muhimu wanasiasa wakashindana kwa hoja kwa kutofautisha kati ya siasa na propaganda .

“Katika uchaguzi wa mwaka huu ni rai yetu vyama tushindane kwa hoja za msingi tutofautishe kati ya siasa na propaganda, sisi tunazungumza siasa na siasa ni ustawi wa taifa na hakuna siasa ya kumtukana mwenzako matusi, hakuna siasa ya kumtoa mwenzako ngeu.” Ameongeza Mbatia

Kwa Upande wake mtia nia ya Ubunge kupitia NCCRA MAGEUZI katika Jimbo la Rombo, Joseph Selasini amesema kuwa vyama vingi ya siasa vinaingia kwenye matatizo ya aina tofauti na kuvifanya visisonge mbele kwa sababu havitengenezwi kwa misingi ya taasisi na hivyo kufa au kutofikiwa malengo yaliyokusudiwa na vyama hivyo.

“Naamini NCCRA MAGEUZI ni taasisi ya wananchi, kwa hiyo nawaomba kuanzia leo muache kusema chama hiki ni cha Mbatia, hiki chama sio mali ya Mbatia, bali Mbatia ni Mwenyekiti wa tatu tangu chama kuanzishwa, na mkisema siku moja chama cha Selasini nitakukamata kwelikweli, hakuna chama cha mtu na chama kitakachoingia madarakani ni chama cha wananchi na sio mali ya mtu.” Amesisitiza Selasini

Kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika October 25 mwaka huu tayari wagombea kutoka vyama mbalimbali wameshaanza kujitokeza kutia ya kugombea katika nafasi za uongozi katika maeneo mbalimbali nchini na hii ikiashiria uhuru na demokrasia kwa kila mwenye nia, uwezo, ushawishi bila kujali itikadi za vyama anapata nafasi ya kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi.