Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
WATU wawili wakazi wa Chapakazi Mji mdogo wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya Mjini wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kughushi nyaraka kwa kutapeli watu kwa kutumia jina la “Mo Dewji foundation.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Benjamin Kuzaga amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Oktoba 22, mwaka huu katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Altas iliyopo Mji Mdogo wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya Mjini hii ni kutokana na misako inayooendelea maeneo mbalimbali.
Kamanda Kuzaga amewataja watuhumiwa hao kuwa ni ,Sarael Geshon (19) na Christiani Erasto (21) ambao wote ni wakazi wa Chapakazi ambao walikamatwa wakiwa katika nyumba hiyo ya kulala wageni.
Amesema watuhumiwa hao walikutwa wakiwa na simu za mkononi smart phone 6, simu ndogo 3, line za simu za mtandao wa Vodacom 10, Tigo 2 na Airtel 3 zenye usajili wa majina tofauti wakizitumia kuibia watu mbalimbali kwa kutoa machapisho ya uongo kwamba wanatoa mikopo kupitia “Mo Dewji Foundation”.
“Watuhumiwa wamekuwa wakighushi kwa njia ya kompyuta kitambulisho cha NIDA, Tin ya TRA, leseni ya biashara na usajili wa Brela kwa jina la “Mo dewji foundation na kisha kutapeli watu wakidai kutoa mikopo kwa riba nafuu,”ameeleza Kamanda huyo.
Pia ameeleza kuwa watuhumiwa hao wamekiri kutekeleza matukio ya utapeli katika maeneo mbalimbali na kujipatia kipato isivyo halali.
Mmoja wa wakazi wa Uyole jijini Mbeya, Baraka Atupele amesema watu kama hao wamekuwa wengi kwenye jamii ambao wamekuwa wakitumia majina ya watu wakubwa kutapeli watu na kujipatia fedha kwa njia isiyo halali .
“Nalipongeza jeshi la polisi kwa jitihada hizi,ombi letu sisi wananchi polisi iongoze nguvu ya msako kwani watu wa hivyo kwenye jamii wapo wengi ambao wamekutwa wakitumia kivuli cha viongozi wakubwa kutoka taasisi mbalimbali,”amesema Baraka.
More Stories
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake