January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbaroni kwa tuhuma za kumchoma moto binti wa kazi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Christina Shiriri kwa jina maarufu Manka,(43), mfanyabiashara na mkazi wa Usagara, wilaya ya Misungwi mkoani hapa kwa tuhuma za kumfanyia ukatili mfanyakazi wake wa ndani Grace Joseph,(17) mkazi wa Kijiji cha Nyalwigo, wilayani humo kwa kumwagia mafuta ya taa mwilini kisha kumchoma moto akimtuhumu kumwibia fedha kiasi cha Tsh. 161,000.

Akizungumzia tukio hilo Juni 5,mwaka huu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbroad Mutafungwa, ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Juni 4,2024 muda wa 02:00hr katika Kata na Tarafa ya
Usagara Wilaya ya Misungwi ambapo Christina Shiriri alidai kuibiwa fedha zake alizokuwa amehifadhi chumbani kwake na alipomuuliza binti yake wa kazi alikiri kuchukua fedha hizo na kuamua kumrejeshea.

Kwa mujibu wa DCP.Mutafungwa ameeleza kuwa vaada ya kurejeshewa fedha hizo Christina Shiriri aliamua kumfanyia ukatili binti huyo kwa kumchoma moto mikono yote miwili, tumboni pamoja na mapaja yake yote mawili.

“Grace ambaye ni majeruhi amepelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa ajili ya matibabu huku mtuhumiwa akiendelea kuhojiwa kwa kina na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika,”.

Hata hivyo jeshi hilo linatoa rai kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi wakati wanapowatuhumu watu wanaofanya makosa,badala yake wawafikishe kwenye vyombo vya sheria kwa ajili ya hatua za kisheria, pia waendelee kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu i ili ziweze kufanyiwa kazi.