November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbaroni kwa tuhuma za kughushi vyeti na leseni za udereva

Na.Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza, linawashikilia watu watano wakiwemo Mkufunzi wa Chuo cha Udereva Nyanza na Mwalimu wa Chuo cha Udereva Chanila, wakidaiwa kuwa watuhumiwa sugu wa makosa ya kugushi vyeti vya udereva,leseni za udereva na kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Akithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao sugu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Wilbrod Mutafungwa amesema walikamatwa kwa nyakati tofauti na maeneo tofauti katika Wilaya za Nyamagana na Ilemela jijini humo.

Amesema Julai 25,mwaka huu, walimkamata Essau Yakobo (26), mkazi wa Mecco Kaskazini, wilayani Ilemela, akiwa na vyeti na leseni za udereva vya kughushi vikiwa na majina, namba,vivuli mbalimbali vya leseni na vyeti,picha na barua mbalimbali za polisi zikiwa zimeghushiwa saini ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa Mwanza.

Mutafungwa amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya kukamatwa John Msemo (45),Ofisa Mauzo wa kampuni ya Chrolide Exide,aliyekwenda polisi kuhakiki cheti cha udereva na daraja la leseni yake akiwa na barua iliyoghushiwa saini Julai 5, mwaka huu, na kudai alivipata kwa Mkufunzi wa Chuo cha Udereva Nyanza,Sixmond George (48),mkazi wa Igoma, baada ya kumpatia fedha.

Alimataja mtuhumiwa mwingine Samwel Bose(47), mkazi wa Ibanda Juu Ilemela na Mwalimu wa Chuo cha Udereva Chanila jijini Mwanza, alikamatwa akiwa na barua ya kughushi ya uhakiki wa leseni kutoka jeshi la polisi.

“Barua hizo za polisi zilizoghushiwa wamekuwa wakizitumia kuwadanya wananchi na kuwahadaa wananchi na kuwatengenezea vyeti batili, tumefanikiwa kunasa mtandao wa wahalifu hao ukiwa na vifaa wanavyotumia kughushi nyaraka hizo ikiwemo printa moja aina ya Epson,kompyuta moja aina ya HP na flash mbili,”amesema Mutafungwa.

Kamanda huyo wa polisi amesema kuwa Julai 27,mwaka huu, majira ya 1:00 asubuhi,katika Bandari ya Mwanza Kaskazini,watuhumiwa wawili,Abdulahim Karungila (41), mkazi wa Bukoba mjini na Heri Kabuya (36)mkazi wa Kyaya, Kata ya Kahororo walitiwa mbaroni kwa tuhuma za vitendo vya uhalifu mtandaoni.

Kwa mujibu wa Mutafungwa watuhumiwa hao walikutwa na nyakara za watumishi wastaafu serikali zikiwa katika mfumo wa machapisho mbalimbali pamoja na laini mbalimbali za simu.

“Watuhumiwa hao katika mahojiano wamekiri kuhusika na vitendo vya uhalifu mitandaoni kwa kuwapigia simu watumishi waliostaafu ambao huwatajia kumbukumbu zao za daftari la utumishi na kuwataka wawatumie fedha wawarekebishie hizo, taarifa”amesema

Pia jeshi la polisi katika uchunguzi wa awali limebaini kuwa watuhumiwa maarufu ‘tuma kwa namba hii’ uhalifu wao wamekuwa wakiufanya katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Dar es Salaam, hivyo watafikishwa mahakamani pamoja na wenzao baada ya kukiri makosa yao ili sheria ichukue mkondo wake.