Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga
JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia mkazi wa mtaa wa Nyasubi wilayani Kahama mkoani humo kwa tuhuma ya kumbaka mtoto wake wa kike ambaye ni wa kufikia(wa kambo).
Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP Janeth Magomi amemtaja mtuhumiwa huyo ambaye amekamatwa kuwa ni Mseveni Mchele (40) anayetuhumiwa kuhusika kumbaka mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa miaka 12 anayesoma darasa la saba.
Kamanda Magomi amefafanua kuwa hivi sasa Polisi inaendelea na upelelezi wa kina na utakapokamilika mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu shitaka lake linalomkabili.
Ameeleza kuwa kitendo ambacho kimefanywa na mtuhumiwa huyo ni kinyume na maadili ya kitanzania hasa ikizingatiwa kuwa mtoto aliyembaka ni mwanae japokuwa ni wa kufikia.
Hivyo ametoa wito kwa wazazi na walezi wa watoto kutokengeuka katika suala zima la malezi ya watoto na wahakikishe wanatimiza wajibu wao kwa kuwalinda ili kuwaepusha na vitendo vyovyote vya ukatili dhidi yao na wao wenyewe wasiwe chanzo cha kuwafanyia ukatili.
Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Abrahaman Nuru, ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo alikiri kutenda kosa hilo ambapo hata hivyo alidai kilichosababisha ni kuzidiwa na ulevi na hivyo ilibidi wampeleke kituo cha Polisi.
Nuru ameendelea kufafanua kuwa baada ya mtuhumiwa kufikishwa polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa waliamua mtoto aliyebakwa apelekwe hospitali kwa ajili ya kupimwa ambako matokeo yalionesha aliingiliwa.
Katika mahojiano na waandishi wa habari mhanga wa tukio hilo (jina limehifadhiwa) amekiri kubakwa na baba yake wa kufikia na kufafanua kuwa kabla ya kubakwa alipewa chips na kinywaji chenye rangi nyeupe asili ya kilevi na alilazimishwa akinywe akiambiwa ni tiba ya ugonjwa wa U.T.I.
Ameendelea kueleza kuwa tabia ya baba yake kumletea chips na kumlazimisha kunywa vimiminika hivyo ilianza mara baada ya mama yake mzazi kusafiri kwenda mkoani Morogoro kwa ajili ya matibabu na kwamba baada ya kuvinywa hujikuta amelewa huku akiwa chumbani kwa baba yake huyo wa kambo akiwa hana nguo.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini