December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP. Muliro Jumanne

Mbaroni akituhumiwa kumuua kikongwe wa miaka 78

Judith Ferdinand, Mwanza

MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Rodha Shabani (27), Mkazi wa Kijiji cha Mwankali Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya bibi kizee aliyafahamika kwa jina la Ndebeto Kakula(78).

Tukio hilo lililotokea Aprili 29,2020 saa 2:20 (08:20 hrs) asubuhi baada ya mtuhumiwa huyo kumkata na kitu chenye ncha kali ambacho baadae kilibainika kuwa ni panga sehemu ya shingoni upande wa kulia wakati kikongwe huyo akitoka kisimani kuchota maji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP. Muliro Jumanne, amesema, Mei 2, saa 8:00 (02:00 hrs) usiku katika kitongoji cha Imalange Kijiji cha Mwanangwa Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza walimkamata mtuhumiwa huyo.

ACP. Muliro amesema, tukio hilo lilitokea baada ya mganga wa kienyeji aliyetambulika kwa jina la Muhangwa Paul kumpigia ramli chonganoshi mtuhumiwa aliye muua bibi kizee huyo kwa madai ya kuwa aliwaroga watoto wake wawili na kusababisha vifo vyao.

Upelelezi umewezesha kukamatwa kwa mganga huyo wa kienyeji pamoja na panga lililotumika kwenye uhalifu huo na tayari upepezi wa shauri hilo umekamilika kwa asilimia 90 na watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.