Na Khadija Bagasha, Timesmajira Online Tanga
Waziri wa Ujenzi na uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya kutoka Tungamaa, Mkwaja hadi Mkange wilayani Bagamoyo yenye urefu wa kilomita 95.2 kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara hiyo ili ikamilike kwa wakati na wananchi waweze kunufaika.
Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo wakati akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani- Saadan hadi Bagamoyo mapema hii leo.
Aidha Waziri Profesa Mbarawa amesema mkandarasi huyo hana kisingizio chochote cha kazi kusimama kwakuwa serikali imeshamlipa fedha kwa asilimia 30 za fedha zote.
“Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya mradi huu , siyo sahihi kuchelewa kutekeleza mradi huu, kama hamtamaliza kwa wakati tutawa Penalize,” amesema Profesa Mbarawa.
Waziri alikuwa akikagua maendeleo ya ujenzi huo ambao hata hivyo hakufurahishwa na kasi ya ujenzi Inavyoendelea na akamuagiza mhandisi mshauri wa kampuni ya Beza kumpa onyo la maandishi kila hatua ya ucheleweshaji inapotokea.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo unaojengwa na serikali na mkopo nafuu wa benki ya Afrika (ADB) kwa shilingi Bilioni 94.2, Meneja wa Wakala wa barabara (TANROADS) Mkoa wa Tanga, mhandisi Eliazary Rweikiza amesema mradi huo ulioanza kujengwa Aprili mosi 2022 utatekelezwa kwa miezi 36 hadi Machi 31 2025, utakamilika.
Hata hivyo, amesema mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Kichina ya Railway 15 bureau Group, umekumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mkandarasi kuwa na vifaa vichache vya ujenzi wa barabara.
Amesema pia mkandarasi huyo kutonunua vifaa vya ujenzi (material) vya kutosha kama mafuta, saruji, nondo na kusababisha kazi kusimama kila mara kutokana na kukosekana vifaa hivyo.
Meneja huyo wa Tanroad amesema wamempa ushauri mkandarasi huyo kuwa aongeze mitambo ya kazi pamoja na kuongeza masaa ya kufanya kazi kwa kuwa yupo nyuma kwa asilimia 12.
“Lakini pia mheshimiwa Waziri tumempa ushauri kwamba alete mitambo ya kuweka lami na pia fedha anazolipwa na serikali wazitumie kwa mradi huu siyo wazipeleke kwenye miradi mingine,” amesema Meneja huyo.
Meneja wa mradi huo Pong Xian Ping alimhakikishia Waziri kuwa watamaliza kwa wakati na kwamba tayari vifaa vya ujenzi vinatarajia kufika nchini baada ya siku kumi kutoka Afrika Kusini.
More Stories
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake