Na Esther Macha,Timesmajira Online. Mbarali
SERIKALI wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya, imepiga marufuku matrekta ya mkono (Powertiler) kutembea usiku na kuonekana kwenye barabara kuu kwani vyombo hivyo, vimekuwa vikisababisha matukio ya ajali za kujirudia mara kwa mara na kusababisha kuwepo kwa ajali na vifo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune wakati wa kikao cha kawaida na askari wa Jeshi la Polisi, kilichofanyika katika Ukumbi wa Polisi Rujewa lengo likiwa ni kukumbusha majukumu na wajibu na maadili ya jeshi hilo.
‘’Kuna watu wengi wanapoteza maisha kutokana na vyombo vya moto tulivyonavyo ambavyo havijasajiliwa, tusiruhusu powertiler kutembea jioni kuanzia saa 12 na kwenye barabara kuu, kwani tukiruhusu kutembea kila sehemu tutakuwa tunahatarisha maisha ya wananchi,” amesema.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya, amewapongeza askari wa Usalama barabarani kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya katika kuhakikisha, wanapunguza uwezekano wa kutokea ajali barabarani.
Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbarali, SSP Harod Mushi amesema wamepokea maelekezo yote yaliyotewa na wanakwenda kuyafanyia kazi kwa mujibu wa sheria.
Katika kikao hicho Mkuu huyo wa Wilaya ameambatana na Kamati ya Usalama Wilaya ya Mbarali.
More Stories
Wizara ya Nishati yawasilisha utekelezaji wa bajeti 2024/2025 kwa Kamati ya kudumu ya bunge Nishati na Madini
Watanzania milioni 13.5 kusambaziwa umeme ifikapo 2030 kutoka milioni 5.2 ya sasa
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji