Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbarali
KATIKA kuhakikisha kila mwananchi ananufaika kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imeendelea kushirikiana kwa karibu na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuhakikisha watumishi wa umma hawajihusishi kuwa wanufaika wa mikopo hiyo.
Akizungumza Oktoba 20, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Raymond Mweli, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amerudisha utaratibu wa utoaji mikopo hiyo kwa nia njema ya kuinua wananchi kiuchumi, na kwamba Halmashauri yake imeweka mikakati thabiti kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa.
“Utoaji wa mikopo hii unafuata taratibu maalumu kwa mujibu wa kanuni za usimamizi. Nikiwa Mkurugenzi, nimeshirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama na TAKUKURU kuhakikisha hakuna mtumishi wa umma anayejiweka kuwa mnufaika wa mikopo hii,” amesema Mweli.

Aidha Mweli ameongeza kuwa Halmashauri imekuwa ikiendesha vikao vya mara kwa mara na wadau mbalimbali wakiwemo maofisa wa TAKUKURU, wataalamu wa Halmashauri na viongozi wa kata, ili kuhakikisha kila mwananchi mwenye vigezo anapata mikopo bila vikwazo.
Aidha, Mweli ametoa onyo kwa watumishi wa umma au wataalamu watakaobainika kukwamisha wananchi kupata mikopo, akisema hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.
“Tunafuata sheria kuhakikisha mikopo hii inatolewa kwa mujibu wa kanuni, na tumekuwa tukitoa elimu kwa wakopaji kabla ya kuchukua mikopo ili wawe na uelewa wa namna bora ya kuitumia na kuirejesha kwa wakati,” amesisitiza Mweli.
Kuhusu sekta ya kilimo, Mweli amesema zaidi ya asilimia 80 ya uchumi wa wananchi wa Mbarali unategemea kilimo, hivyo Halmashauri imeamua kutoa kipaumbele kwa vikundi vinavyojishughulisha na kilimo katika upatikanaji wa mikopo hiyo.
“Vikundi vingi vya wanawake na vijana vinaomba mikopo kupitia sekta ya kilimo, na tumetoa maelekezo kwamba vipewe kipaumbele, kwa kuwa kilimo ndicho kinachochangia sehemu kubwa ya mapato ya Halmashauri,” amesema.
Kwa upande wake, Gwimile Ibrahim, mkulima wa mpunga kutoka Kata ya Ubaruku, amesema mikopo hiyo imemsaidia kuboresha maisha yake, ikiwemo kumwezesha kusomesha watoto na kuimarisha kipato cha familia.
“Mikopo hii imenisaidia kufika hapa nilipo. Nimekuwa nikirejesha kwa wakati ili wengine pia wanufaike. Naomba wakulima wenzangu tuwe waaminifu, tusimuangushe Mkurugenzi wetu ambaye ametupa kipaumbele,” amesema Gwimile.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi