March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbarali yaendelea kuzitambua shule shikizi

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbarali

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imesema inazitambua na kuviimarisha vituo shikizi 23 vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na tayari ipo katika hatua za kuhakikisha vituo hivyo vinasajiliwa kwa mujibu wa sheria ili ziweze kukidhi sifa na kusajiliwa kisheria na kuwa Shule rasmi.

Kwa mwaka 2026 vituo 5 vimeombewa Usajili kuwa Shule rasmi za Msingi ili kusogeza huduma ya Elimu kwa wananchi.

Akizungumza na Timesmajira Online Februari 17, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Raymond Mweli, amesema baadhi ya vijiji na vitongoji vilivyopo pembezoni mwa wilaya havina shule rasmi za msingi au sekondari, hali iliyosababisha kuanzishwa kwa shule shikizi ili kuwahudumia watoto wa maeneo hayo.

Amesema halmashauri haijaanzisha rasmi shule mpya za msingi au sekondari, bali inavitambua Vituo shikizi vilivyopo na inaendelea na utaratibu wa kuviimarisha kwa Miundombinu kwa awamu ili ziweze kusajiliwa kisheria kuwa Shule rasmi.

“Hatujaanzisha rasmi shule za msingi au sekondari, bali vipo Vituo shikizi ambavyo tunavitambua na tupo katika utaratibu wa kuhakikisha vinasajiliwa kwa mujibu wa sheria. Lengo si usajili tu, bali pia kupeleka rasilimali watu, hususan walimu, na kuhakikisha huduma zote zinazotolewa katika shule mama pia zinapatikana pia katika shule shikizi kuanzia Darasa la Awali hadi Darasa III,”
amesema Mweli.

Ameongeza kuwa halmashauri inaendelea kutathmini ubora wa elimu inayotolewa katika Vituo hivyo kwa kuwapeleka wataalamu kufanya tathmini na kuwasilisha taarifa katika mamlaka husika kwa ajili ya maboresho zaidi tukilenga kuzifanya kuwa Shule rasmi.

Kwa sasa, amesema , Vituo vyote shikizi vya elimu ya msingi katika wilaya hiyo vimeendelea kutambuliwa rasmi na vinaendelea kutoa huduma kwa wanafunzi, huku zoezi la kupeleka walimu likiendelea ili kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora unazingatiwa.

Aidha Mweli amesema Kata zisizo na Sekondari ziwekewa mpango wa kuwa na Sekondari.

Akizungumzia bajeti, Mweli amesema halmashauri itaendelea kutenga fedha kadri mapato ya ndani yatakavyoruhusu ili kuimarisha miundombinu ya shule hizo, ikiwemo madarasa, vyoo na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Bajeti ya 2026/27 Tsh.100,000,000/= tumetenga ili kukamilisha vyumba 8 kwenye vituo shikizi 8 kupitia Mapato ya ndani ya Halmashauri.

Amesema pamoja na kutegemea mapato ya ndani, halmashauri pia ina mpango wa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wenye nia njema kusaidia kuboresha shule shikizi.

“Tunatambua kuwa tuna majukumu mengi ya maendeleo kupitia mapato ya ndani, lakini Vituo shikizi ni moja ya maeneo ya kipaumbele. Tunaamini kwa kushirikiana na wadau, tutaweza kuziimarisha zaidi,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Rujewa, Jeremiah Makao, amesema uwepo wa shule shikizi umesaidia kwa kiasi kikubwa watoto wa maeneo ya mbali ambao awali walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata shule.

Amesema jitihada za halmashauri kupeleka walimu na kuboresha mazingira ya kujifunzia zimeleta tija kubwa katika utoaji wa elimu, huku akisisitiza umuhimu wa kuharakisha usajili wa shule hizo ili ziweze kupata stahiki zote za kisheria.