November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mavunde:Utoroshaji madini unaikosesha serikali mapato

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WAZIRI wa Madini,Anthony Mavunde amewataka wadau wote wa Sekta ya Madini nchini kutojihusisha na vitendo vya utoroshaji madini katika maeneo yoyote yenye uchimbaji, uhifadhi na uuzaji kwani kwa kufanya hivyo kunaikosesha Serikali kupata mapato yatokanayo na rasilimali madini.

Mavunde amesema hayo jijini hapa Oktoba 19, 2023 wakati akizungumza na Wanachama wa Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMMATA)ambapo amesema kuwa Serikali ina mipango mingi katika kuendeleza Sekta ya Madini lengo likiwa ifikapo mwaka 2025 sekta hii kuchangia asilimia zaidi ya kumi (10%) katika pato la Taifa (GDP) kama mpango wa Maendeleo wa Dira ya Taifa 2025 unavyoelekeza.

Ameeleza mchango wa madini katika Pato la Taifa katika Mwaka 2022/2023 kuwa Sekta ya Madini ilikusanya zaidi ya shilingi Bilioni 600 huku asilimia 40 ikichangiwa na wachimbaji wadogo , wafanyabiashara wa madini wa ndani na Broka.

Aidha ameeleza mzunguko wa fedha katika mnyororo mzima wa Sekta ya Madini,amesema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliweza kukusanya mapato ya kodi ya ndani ya kiasi cha shilingi trilioni mbili kulingana na mzunguko wa fedha katika masoko ya ndani ya madini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHAMMATA Jeremia Kituyo amesema kuwa ili kuondokana na utoroshaji wa madini nchini ni vyema Serikali ikaja na mpango wa kukata leseni kwa mfumo wa kikanda ili kutoa wigo mpana kwa wafanyabiashara kutoka kanda moja na nyingine.

Kituyo amesema kuwa ni muda muafaka wa Serikali kuweka biashara ya madini kuwa huria katika masoko ya madini hususan katika minada ili kuwezesha bei kuwa shindani katika masoko ya madini.

Pamoja na hayo ameeleza lengo la kuanzishwa kwa CHAMMATA amesema kuwa ni pamoja na kuwaunganisha wafanyabiashara wa madini na Serikali pamoja na kutetea na kusimamia haki za wafanyabiashara wa madini nchini.