December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mavunde:Sitakuwa na huruma kwa yeyote atakayetorosha madini nje ya nchi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

WAZIRI wa Madini,Anthony Mavunde amesema
kuwa ili kuhakikisha nchi inanufaika na rasilimali za Madini hatakuwa na huruma kwa mtu yeyote atakayebainika kutorosha Madini nje ya nchi kwani hatasita kumchukulia hatua za Kisheria.

Mavunde amesema hayo jijini hapa leo Septemba 11,2023 wakati wa kikao Cha pamoja kati ya Wachimbaji wadogo chini ya Mwamvuli wa FEMATA.

Ameseama kuwa hataangalia sura ya mtu wala cheo kwa yeyote ambaye atabainika kutorosha Madini nje ya nchi kutokana na kuwepo kwa wimbi hilo huku akibainisha Mikakati mbalimbali ambayo itaongeza Pato la Uchumi wa Nchi pamoja na Wachimbaji kwa ujumla.

“Najua Kuna utoroshaji mkubwa sana wa Madini lakini Kuna kazi kubwa inayofanyika ya kuzuia Vitendo hivyo ili nchi iweze kunufaika na Madini kutokana na dhamana niliyopewa lazima nisimamie Sheria,

“Madini ya Kimkakati, mahitaji ya dunia leo ni tani milioni 10, kufikia mwaka 2050 mahitaji yatakuwa tani laki moja na nusu, sisi Tanzania tunabahati na kuwa nayo, tunaenda kuyapa kipaumbele ili utajiri huu tunufaike nao,” amesema Mavunde.

Aidha ameeleza Mikakati atakayoitekeleza ambayo ni Ajenda ya 2030 Madini ni maisha na utajiri ambapo ataijengea uwezo Taasisi ya jiolojiana utafiti wa Madini nchini (GST)kwani huo ndio Moyo wa Madini kuhakikisha inafanya utafiti wa Madini ili kutoa taarifa sahihi za kijilojia na kuweza kufikia malengo yao.

Mavunde ameeleza kuwa ili kufanya utafiti huo ,mwelekeo wake chini ya maelekezo ya Rais anataka kufanya utafiti katika maeneo yote ili kupata taarifa za jiolojia maeneo yote yenye miamba na uwepo wa Madini na kutimiza azma ya Serikali katika ukuaji wa Sekta hiyo.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa ipo changamoto ya baadhi ya Wachimbaji kutopeleka dhahabu kwenye viwanda vya kusafishia dhahabu hivyo katika kutatua hilo, Serikali itatoa mikopo kupitia wamiliki wa viwanda hivyo ili wachimbaji wanapokuwa na dhahabu zao wapeleke kusafisha kwenye viwanda hivyo ili kuongeza mzunguko wa fedha.

Katika hatua nyingine Mavunde amesema kuwa kutokana na kazi kubwa inayofanyika na GST watajenga Maabara ya kisasa ili kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amewataka wachimbaji, wafanyabiashara na watu wote wanaojihusisha na mnyororo mzima wa Sekta ya Madini kufuata utaratibu kwa kulipa kodi sambamba na kuepuka utoroshaji Madini ili Sekta ifikie lengo lake kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.

Naye Rais wa Shirikisho la Wachimbaji wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA)John Bina ameeleza changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo suala la Kodi kubwa ya tozo na kushuka kwa bei ya Tanzanite.

Hivyo ameiomba serikali kupunguza kodi katika mitambo inayoingizwa hapa nchini kwa ajili ya kurahisisha uchimbaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi

“Mheshiniwa Waziri tunaomba kupitia wewe Serikali itusaidie kutatua changamoto hizi za tozo pamoja na gharama kubwa ya umeme pia tujengewe Hospitali pale Merelani kutona na uwepo wa vumbi,”amesisitiza.