Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WIZARA ya Madini imesema mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 11 robo ya kwanza ya mwaka 2025 hadi asilimia 12 robo ya pili, hatua inayoonesha kuimarika kwa sekta hiyo nchini.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Januari 26,2026 na Waziri wa Madini, Antony Mavunde,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi chake cha pili ambapo amesema mchango huo umeongezeka kwa kasi ikilinganishwa na asilimia 6.8 mwaka 2020 na asilimia 10.1 mwaka 2024.

Amesema kati ya Julai na Desemba 2025, tani 14.66 za dhahabu zenye thamani ya Sh. trilioni 3.75 ziliuzwa katika viwanda vya kusafisha dhahabu nchini, huku hadi Desemba 2025 Serikali kupitia BoT ikinunua tani 17.03 zenye thamani ya Sh. trilioni 4.97, hatua iliyoimarisha akiba ya dhahabu ya Taifa.
“Novemba 2025 hadi Januari 25, 2026, Wizara ya Madini ilikusanya Sh. bilioni 311.80 sawa na asilimia 111 ya lengo, na Julai hadi Desemba 2025 ikakusanya Sh. bilioni 653.94 sawa na asilimia 108.99 ya lengo la kipindi hicho. Mafanikio hayo yametokana na maboresho ya sheria, usimamizi wa leseni, udhibiti wa biashara ya madini na mapambano dhidi ya utoroshaji wa madini.”amesema.

Pamoja na hayo Mavunde amesema Wizara ya Madini inaelekea kutumia mfumo wa E-Licensing, ambao hautahitaji waombaji kufika wizarani. Kupitia mfumo huo, mwombaji atapatiwa leseni na ndani ya kipindi cha miezi mitatu atatakiwa kuwasilisha taarifa ya utafiti wake.
“Wizara imefanikiwa kuratibu utoaji wa leseni 12,130, sawa na asilimia 117.8 ya lengo la mwaka wa fedha 2024/2025. Aidha, katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, jumla ya leseni 8,418 zilitolewa sawa na asilimia 147 ya lengo la kipindi husika,” Amesema Waziri Mavunde
” Kuanzia Novemba 2025 hadi Januari 2026, leseni 2,376 zilitolewa ambapo katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, Wizara ilifuta leseni 73 za utafutaji na uchimbaji madini kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo kutokuendelezwa kwa maeneo husika, ” Amesema


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina