March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maumivu Sugu ya Mgongo, Nyonga na Magoti yazidi kuwatesa Wananchi wa umri wa kati – MOI yatoa Tumaini jipya 


Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma

KATIKA  kuadhimisha wiki ya utumishi wa umma, Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imeshiriki maadhimisho kwa  kutoa huduma na ushauri kuhusu matatizo ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.

Akizungumza katika banda la Taasisi hiyo  katika viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma leo Juni 18,2025  Daktari Bingwa wa upasuaji wa mifupa kutoka MOI, Dkt. Tumaini Minja, amesema kuwa tangu maonyesho yalipoanza Juni 16 mpaka sasa wameshawaona wagonjwa zaidi ya 70 na bado wanaendelea kuwaona na kuwahudumia wagonjwa.

Dkt. Minja amesema kuwa idadi kubwa ya wagonjwa waliowahudumia wanatoka katika mkoa wa Dodoma pamoja na mikoa ya jirani ya inayozunguka mkoa huo huku taatizo kubwa lililogundulika ni maumivu sugu ya mgongo, nyonga na magoti.

Kwa mujibu wa Dkt.Minja magonjwa hayo mara nyingi huchangiwa na uchakavu wa pingili na viungo kutokana na umri mkubwa na uzito wa mwili kupita kiasi.

“Miongoni mwa wagonjwa tuliowahudumia pia wapo  wale waliowahi kufanyiwa upasuaji MOI jijini Dar es Salaam,baadhi yao walipata matibabu ya kawaida bila upasuaji na sasa wanaendelea vizuri. Amesema na kuongeza kuwa

“Hii inaonesha kuwa huduma tunazotoa zina matokeo chanya na tunajivunia kuona wagonjwa wetu wakiendelea vizuri na tumewashauri waendelee na maisha ya kawaida,”

Aidha Dkt.Minja amesema,kundi kubwa la wagonjwa wanaopata matatizo haya liko kati ya umri wa miaka 45 hadi 60 huku akisema mtindo wa maisha kwa maana ya shughuli za kila siku nao unachangia tatizo la uchakavu wa viungo.

Kwa mujibu wa Dkt. Minja, matatizo haya yanatibika iwapo yatawahiwa. Wagonjwa wanaweza kupewa matibabu ya dawa, mazoezi au kufanyiwa upasuaji kulingana na kiwango cha tatizo.

“Kwa mfano, wagonjwa wenye uchakavu wa nyonga na magoti wanaweza kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha viungo hivyo na kurejea katika hali nzuri kabisa ya kiafya,” alisema.

Alisisitiza kuwa elimu ya afya ya mifupa ni jambo muhimu kwa jamii, na akatoa wito kwa wakazi wa Dodoma na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi katika banda la MOI kupata huduma, ushauri na vipimo vya awali.

“Hii ni fursa ya kipekee, wananchi waitumie kujifunza namna ya kujikinga na magonjwa haya ya mifupa ambayo yamekuwa kikwazo kwa maisha ya watu wengi,” aliongeza.

Huduma zinazotolewa na MOI katika maonesho haya ni pamoja na uchunguzi wa awali wa matatizo ya viungo, ushauri wa kitaalamu kuhusu tiba sahihi, na uhamasishaji juu ya njia bora za kujikinga na matatizo ya mifupa.

 Dkt. Minja amesema taasisi yao itaendelea kufikisha huduma kwa wananchi wengi zaidi nchini kote.