December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Matumizi umeme wa gesi yafikia asilimia 64

Na Penina Malundo

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema asilimia 64 ya umeme unaotumika nchini unazalishwa kwa kutumia gesi asilia, huku ukifuatiwa na ule unaozalishwa kwa kutumia vyanzo vya maji na vyanzo vingine vidogo.

Hayo yalisemwa juzi na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea banda la TANESCO katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Alisema tangu ugunduzi wa gesi nchini matumizi ambayo yametumika ni kuzalisha umeme ambapo kwa sasa karibu asilimia 64 ya umeme wote unaotumika nchini unazalishwa kwa kutumia gesi hiyo asilia.

Mramba alisema maji nacho ni miongoni mwa chanzo kinachozalisha Umeme kwa kushika nafasi ya pili, huku vyanzo vingine vikichangia uzalishaji umeme kwa kiasi kidogo.

Alisema kwa sasa mazungumzo baina ya serikali kuhusu mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia (LNG) yamefikia mwishoni na sasa wapo kwenye hatua zinazofuatia.

Alitaja manufaa yanayotarajiwa ni kuanza kunufaika na gesi ambayo imegunduliwa kwa muda mrefu na haijaweza kutumika kwa kiasi kikubwa.

Alisema mradi wa LNG ndio utakaowezsha gesi ya Tanzania kuuzwa nje ya nchi na kwamba zipo namna chache za kutekeleza jambo, ikiwemo kutengeneza mabomba na kusafirisha gesi hiyo kwenda nchi za karibu.

“Njia nyingine ni kuigandisha ili iwe katika hali ya kimiminika na hivyo kupakiwa kwenye meli kubwa na kupelekwa nchi za ngambo, hatua ambayo itailetea Tanzania fedha za kigeni.” alisema na kuongeza;

“Sasa tunapokuwa na miradi mikubwa kama hii tunapaswa kujiandaa kwani mradi wa LNG utaleta ajira na matumizi mengine ya gesi.”

Alisema wanajiandaa mapema kuanza kutangaza kutoa vitalu kwa wawekezaji mbalimbali wanaofanya utafiti wa kugundua gesi zaidi au mafuta.