KABUL,Mwakilishi maalum wa Marekani katika mazungumzo ya maridhiano ya Afghanistan, Zalmay Khalilzad, amesema kuondoka kwa zaidi ya raia 250 wa kigeni nchini Afghanistan baada ya kukubaliwa na kundi tawala la Taliban ni jambo muhimu.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani, pia amelishukuru shirika la ndege la Qatar lililowasafirisha raia hao wakiwemo raia kadhaa wa Marekani, kutoka uwanja wa ndege wa Kabul.
Khalilzad amesema, Marekani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Qatar, Taliban na wengine ili kuhakikisha njia salama zinatumika kuwahamisha wale wote wanaotaka kuondoka Afghanistan.
Zoezi la kijeshi la kuwaokoa raia wa kigeni na Waafghanistan waliofanya kazi na vikosi vya kigeni lilianza baada ya kundi la Taliban kuudhibiti mji mkuu, Kabul katikati ya mwezi Agosti.
Wakati huo huo,Ofisi ya Msemaji wa Shirika la Ndege la Kimataifa la Pakistan imeliambia shirika la habari la AFP kwamba, wataanzisha tena safari za ndege kutoka Islamabad hadi Kabul wiki ijayo.
Hiyo ikiwa ni safari ya kwanza ya kigeni kufanyika katika uwanja wa ndege wa Kabul, tangu kundi la Taliban lilipochukua madaraka mwezi uliyopita.
Uwanja huo wa ndege uliharibiwa vibaya wakati wa zoezi lililojaa vurugu la kuwaondoa zaidi ya watu 120,000 waliotaka kuihama nchi hiyo, kwa kuhofia utawala wa Taliban.
Zoezi hilo lilimalizika Agosti 30 baada ya wanajeshi wa Marekani kuondoka Afghanistan. Kundi la Taliban limekuwa likijaribu kuufufua tena uwanja huo wa ndege kwa usaidizi wa wataalamu wa kiufundi kutoka Qatar ili uweze kutoa huduma.
More Stories
Dk. Mpango amwakilisha Samia sherehe za Uhuru wa Lesotho
Samia atangaza Tanzania kumuunga mkono Odinga
Tanzania yaongoza kikao maalum cha nishati safi