November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Matukio ya ulawiti,ubakaji watoto yanavyoathiri ukuaji wao

Joyce Kasiki

MOJA ya changamoto inayowakabili watoto nchini ni uimarishwaji wa ulinzi wao ili kuwasaidia na kuwakinga dhidi ya matukio ya ulawiti na ubakaji dhidi yao.

Matukio hayo yamekuwa yakitokea katika maeneo mbalimbali  hapa nchini ambayo kwa namna moja ama nyingine yanawaathiri watoto kisaikolojia na hivyo kuathiri ukuaji wao kwa ujumla.

Mkoani  Dodoma katika baadhi ya maeneo kumekuwa kunaripotiwa matukio ya kikatili dhidi ya watoto ambayo yanaamsha msukumo wa kuimarisha ulinzi kwa mtoto.

Mtaa wa Hado Kata ya Miyuji ,ni  moja ya mtaa ambao kumeripotiwa baadhi ya matukio ya ukatili wa ulawiti wanayofanyiana watoto wadogo kati ya umri wa miaka mitano na kuendelea , hali ambayo imeibua hofu kwa wakazi wa eneo hilo na hata baadhi kudai vitendo hivyo vimekuwa sugu kwenye eneo hilo.

Kwa mujibu wa Sayansi ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali Mtoto,watoto wadogo wa umri wa miaka sifuri hadi minane,ubongo wao hautakiwi kuathiriwa na aina yoyote ya ukatili,lakini pia umri huo ndio kipindi ambacho ubongo wa mtoto hukua kwa kasi na kwamba vitu anavyojifunza wakati huo haviwezi kuvisahau hata atakapokuwa mkubwa ,hivyo watoto hao wanapaswa kulindwa na kulelewa kwa kufuata kihunzi cha malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wameiomba serikali kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu  ulinzi wa watoto ,malezi na makuzi yao kwa ujumla kwa maslahi mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla .

Jackson Kadebe mkazi wa eneo hilo anasema mtaa huo umekuwa na matukio ya watoto wadogo kufanya vitendo vichafu kutokana  na wazazi kutokuwajibika kwenye suala zima la malezi na makuzi ya watoto wao.

Kadebe ambaye pia ni Balozi wa Shina Namba tatu anasema mara kadhaa matukio hayo yamekuwa yakitokea na kwamba amekuwa mstari wa mbele kukemea na kuwasihi wazazi kuzingatia  eneo la malezi ya watoto.

“Malezi duni ya wazazi kwa watoto wao yanachangia ukosefu wa maadili kwa watoto ,wazazi hatuwadhibiti watoto ,wanaenda kuangalia video chafu kwenye  vibanda umiza .”anasema Kadebe

Akizungumzia suala hilo Mwenyekiti wa Serikali ya   Mtaa Alphaxard Ganyara anasema ,wanaofanya hivyo ni watoto wadogo wanaopaswa kufundishwa na wazazi wao ili waishi katika maali mema.

“Watoto waadhibiwe na wakaripiwe,matukio haya yasiendelee ,utoto urekebishwe kwa kuonywa maana wakiachwa hivi hivi ni hasara kwa jamii na Taifa.” Anasema Ganyara

Mtaalam wa Malezi , Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto  Davis Gisuka anasema, watoto wanapaswa  kulindwa dhidi ya ukatili wowote kwa ajili ya ustawi wa malezi na makuzi yao ambao utawawezesha kufikia ukuaji timilifu.

Anasema ,athari za matukio haya kwa watoto ni kubwa kwani inawaathiri kisaikolojia kwani anayefanya hivyo vitendo ataendelea kufanya hivyo hata atakapokua mkubwa.

“Kwa hiyo viongozi wote kuanzia ngazi za chini kabisa wana wajibu wa kuwalinya watoto dhidi ya matukio yoyote yanayoweza kuathiri ukuaji wao na kuwaelimisha wazazi kuhusu suala la malezi ya watoto na umuhimu wake kwa mtoto mwenyewe,jamii naTaifakwa ujumla.”anasema Davis

Naye Magreth Mukama kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Action for Community Care (ACC) linalotekeleza mradi wa Mtoto Kwanza unaofanya uchechemuzi wa utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto anasema katika utekelezaji wa Mradi huo wamekuwa wakitoa elimu ya malezi na makuzi kwa wazazi na walezi kufuata namna bora ya malezi ya watoto .

“Kama tunavyofahamu katika ukuaji wa mtoto ubongo wake hautakiwi kuathiriwa na kitu chochote ili kumwezesha kuwa na ukuaji timilifu,na ndio maana katika kihunzi cha malezi ya mtoto kuna mambo matano ya kuzingatiwa ikiwemo kuhakikisha anakuwa na afya bora,lishe ya kutosha,ujifunzaji wa awali,ulinzi na usalama pamoja na malezi yenye mwitikio,

“Kwa hiyo mzazi akikosea kwenye eneo moja kati ya hayo inaathiri ukuaji wake na hivyo kufanya mtoto kukosa ukuaji timilifu na hivyo kuongeza tija katika jamii na Taifa kwa ujumla.”anasema Mukama

Mrakibu Msaisizi wa Polisi ,Dawati la Polisi mkoa wa Dodoma Christer Kayombo  anasema, kitengo hicho kimekuwa kikipokea taarifa za matukio hayo na wamekuwa wakiyafanyia kazi kwa kwenda kwenye eneo    matukio hayo yanakofanyika kwa ajili ya kwenda kuona namna ya kusaidia kukomesha matukio hayo.

“Ukiona mtoto anafanya hivyo kwa mwenzie ujue na yeye kuna mtu anamfanyia hivyo,kwa hiyo inakuwa ni ‘chain’, kwa hiyo tunachokifanya ni kufuatilia hadi kujua tatizo limeanzia wapi ili kuliondoa kuanzia lilipoanzia.”anasema Kayombo 

Mkuu wa wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri anasema watoto ni moja kati ya makundi muhimu ambayo yanapaswa kulindwa dhidi ya ukatili wa aina yoyote kwa kuhakikishiwa usalama wao nyakati zote huku akiahidi kushughulikia changamoto ya watoto katika mtaa wa Hado Kata ya Miyuji.

Kwa mujibu wa Programu Jumuishi ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ,takwimu zinaonesha kuongezeka kwa kesi za ukatili kwa watoto katika umri wote ambapo mwaka  2017 kesi 13,457 ziliripotiwa ,mwaka 2018 kesi 14,419 sawa na ongezeko la asilimia 7.2 huku mwaka 2019 kukiwa na kesi 15,980 sawa na ongezeko la asilimia 10.8 .

Shime wazazi na  walezi tuamke na kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya ukatili wa aina yoyote ili waweze kufikia hatua timilifu za ukuaji na hivyo kuleta tija katika nchi.