January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashuka yenye thamani ya milioni 3 yatolewa kusaidia wagonjwa

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

CHAMA cha Ushirika cha Akiba na Mikopo tawi la Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (NEW MZRH SACCOSS) kimetoa msaada wa mashuka 200 yenye thamani ya milioni 3 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.

Msaada huo wa mashuka ni sehemu yake ya huduma kwa jamii kwa kutambua changamoto mbalimbali ambazo hospitali inakutana nazo katika kuwahudumia wagonjwa hospitalini hapo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Mwenyekiti wa NEW MZRH SACCOSS, Emmanuel Nsenye, amesema kuwa anatambua mchango wa uongozi na wataalamu wa hospitali hiyo katika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi na kueleza kuwa msaada huo wa mashuka 200 wenye thamani ya shilingi milioni 3 unatolewa kama sehemu ya wajibu wa chama hicho kwa jamii.

Pamoja na kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali yake katika kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.

“Hii ni kutambua umuhimu wa maendeleo ya huduma za afya hapa nchini, kurudisha kwa jamii yenye uhitaji pia kuendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya hospitali na wadau wa maendeleo,”amesema.

Nsenye ameonesha matumaini ya kuendelea kushirikiana na hospitali hiyo na taasisi nyingine katika kuboresha huduma za afya nchini kwa kutoa msaada utakaosaidia kupunguza changamoto katika utoaji wa huduma za afya hatua ambayo inaonesha nia njema ya NEW MZRH SACCOSS katika kusaidia kuleta maendeleo na mabadiliko chanya katika sekta ya afya nchini.

Naye Mercy Lutumo ambaye ni Muuguzi Mkuu Msaidizi akipokea mashuka hayo kwa niaba ya uongozi wa hospitali hiyo ameipongeza NEW MZRH SACCOSS kwa msaada wa mashuka huku akieleza kuwa msaada huo utasaidia sana kuboresha huduma za afya kwa wagonjwa.

Aidha, Lutumo amewataka wananchi na taasisi mbalimbali kuendelea kuchangia jamii zenye uhitaji ili kuweza kupunguza changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma za kijamii, hususani huduma za afya.

Amesema kwamba, kila mtu anao wajibu wa kusaidia jamii ili kufikia maendeleo na hivyo kuendelea kuwa na taifa lenye afya bora.

“Ni jambo zuri lenye mfano wa kuigwa kwa taasisi zingine ambazo zinatoa huduma kwa jamii waone umuhimu kushiriki katika kutoa mahitaji mbalimbali kwa wahijati katika vituo vya watoto yatima,hospitalini ambavyo vitasaidia katika kupunguza makali ya maisha,”amesema Lutumo.

Amesema kuwa,uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya unawahakikishia wananchi kuwa utaendelea kutoa huduma bora za afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hivyo kuwataka wananchi kuendelea kuitumia hospitali hiyo kwa ajili ya kutatua changamoto zao za kiafya.

Elizabeth Satima, muuguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, ameeleza kuwa msaada huo umekuja kwa wakati muafaka kutokana na ongezeko la wagonjwa ambalo ni matokeo ya maboresho ya miundombinu na upanuzi wa huduma za afya.

Pia ametoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano wa NEW MZRH SACCOSS kwa kutoa misaada kwa hospitali na jamii zenye uhitaji huku akiwahakikishia wadau hao kuwa msaada huo utatumika ipasavyo na utaleta mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.