September 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashujaa saratani walivyosheherekea maisha

*Serikali yahimiza kushikamana kuwasaidia

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

NI Jumapili ya kwanza ya mwezi Juni, mashujaa wa saratani wamekusanyika katika viwanja vya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) wakionekana wenye furaha, baadhi wakicheza muziki, wengine wakiwa wamekaa wakijadiliana mambo mbalimbali.

Ama kwa hakika walionekana wenye furaha japokuwa miongoni mwao ni wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo maarufu hapa nchini kwa tiba ya saratani.

Mara kadhaa viongozi wao wanasikika wakisema kupitia vipaaaza sauti: “Survivour!” (‘Mashujaa!’) na uwanja mzima unalipuka “A celebration of life’ (‘Sheherekea maisha’).

Kwa hakika wanaonekana ni watu wenye furaha ingawa miongoni mwao wanaonekana waliofunga vitambaa kichwani kuonesha wana vidonda na baadhi yao mikononi zilinaonekana sindanu maalumu zilizofungwa na bandeji ambazo hutumika kwa mtu kutundikiwa ili kuongezewa maji au damu mwilini.

Nimekuwa na shauku ya kujua nini sababu ya furaha ya watu hawa, nimekutana na mmoja wa viongozi wao ambaye anajitambulisha kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Shujaa Cancer Foundation (SCF), Gloria Kida.

Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Shujaa Cancer Foundation (SCF), Gloria Kida.

“Hapa tumekusanyika mashujaa wa saratani, ni siku yetu maalumu inayosheherekewa duniani kote. Tumekusanyika hapa kwa pamoja mashujaa wa saratani kutambua waliogundulika na ugonjwa, wanaoishi na ugonjwa na wenye historian a ugonjwa,” Anasema Kida ambaye ambaye anajitambulisha pia kuwa ni miongoni mwa mashujaa.

“Dhumuni kuu la siku hii ya leo ni kuongeza uelewa wa changamoto ambazo wanapitia mashujaa na zaidi ni kushehereka maisha. Tunakutana kupongezana na kupeana moyo juu ya mambo na changamoto mbalimbali zinazotuhusu.
“Bahati nzuri mwaka huu tumekutana chini ya kauli yetu mbiu ya ‘A Celebration of Life’ ikiwa na maaana ni siku yetu maalumu ya ‘kusheherekea maisha.’ Leo ni siku yetu ya kufurahi tu.”

Je, nini maana ya ‘siku ya mashujaa wa saratani? Shujaa wa saratani ni nani?’ Kida anajibu kwa kusema:

“Kwa ufupi ni kusanyiko linahusiana na kuwatambua mashujaa wote wa saratani na kuonesha jamii na ulimwengu kuwa kuna maisha baada yakugundulika na saratani.

“Si hilo tu bali ni wakati ambao wagonjwa wataonesha kuwa baada ya maitibabu kuna matumaini ya hali zao kuwa timilifu au kuwa zawadi ya maisha mapya na yenye furaha na hamasa.”

Katika maadhimisho hayo, Kida anasema mashujaa kadhaa wa saratani hujitokeza kuweka wazi madhila waliyoyapata wakiugua na kutibiwa saratani.

Lengo ni kuelimisha jamii pamoja na wagonjwa wa saratani kuwa kuugua maradhi haya siyo mwisho wa maisha na hatupaswi kuwa wanyonge bali ni wenye furaha.

Anasema wengi wa mashujaa wamepitia changamoto nyingi katika historia ya ugonjwa zikiwamo za gharama kubwa za matibabu, kifurushi pungufu cha afya, ugumu wa maisha, familia kufarakana, wanandoa kutalikiana, kupoteza ajira, kipato kushuka kutokana muda mwingi kutumika kujitibia na familia kufilisika.

Matatizo mengine anayataja kuwa ni athari za kisaikolojia zinazosababishwa na changamoto za kijamii, kifamilia na hata kuugua kwa muda mrefu na hapa mgonjwa anaweza kukatishwa tamaa ya kuishi baada ya mwenza wake ameamua kumuacha na kwenda kuishi na mwingine.

Pamoja na changamoto hizo, sisi tunasema shujaa wa saratani hapaswi kukata tamaa bali kuamini kuwa kuna nafasi ya maisha mengine mazuri sasa na baadae nab ado Mungu yupo pamoja nasi.

“Kwa kweli tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha. Kusema kweli mashujaa wanapitia katika changamoto nyingi ila napenda kuwatia moyo wa kujiamini kuwa wewe ni jasiri, shupavu na ni shujaa.

“Una uwezo wa kupata nguvu na kuinuka na yote kwa msaada wa Mungu na kumuweka mbele, utavuka changamoto zote na kuwa tena mtu mwenye furaha na amani.”

Anasema shujaa akipata nafuu, fursa ya kipekee ni kujiunga katika vikundi vya mashujaa ili kama utakumbana na changamoto, utapata maarifa ya namna ya kuzikabili na kuepuka msongo wa mawazo.

“Changamoto za muda mrefu za tiba zisikukatishe tamaa na kukuondolea furaha yako ya moyoni. Mtumaini Mung una uamini duniani changamoto haziishi na wala siyo za ugonjwa tu.”

Hata hivyo, Kida alisema taasisi ya SCF inatambua juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za afya nchini jambo ambalo limewaletea mapinduzi ya tiba kiasi kwamba huduma ambazo wangepaswa kukimbilia nchi za nje, zinapatikana nchini.

Nani anaweza kuitwa shujaa wa saratani? Kida anasema kuwa katika maadhimisho haya, wanamtambua shujaa wa saratani ni yule anayeishi na historoa ya saratani kutokea alipogundulika mpaka maisha yake yote.

Anasema huanza kuitwa shujaa wa saratani kuanzia pale anapoamua kuanza tiba hospitalini baada ya kugundulika na kuridhia kwa moyo mmoja kuanza kufuata kikamilifu ushauri wa daktarin ili kukabiliana na ugonjwa huo.
“SCF inatoa kipa umbele cha kuwahudumia mashujaa hawa kwa sababu tibe yake si nyepesi kama ilivyo ya magonjwa mengine. Safari ya mgonjwa wa saratani inaanza pale anapogundulika hospitalini ana saratani mpaka anapomaliza tiba ya awali na kuendelea na maisha mapya.

“Maisha haya mapya kwa shujaa wa saratani huwa yanakuwa na mabadiliko makubwa ambayo yanahitaji msaada ili kuweza kuyamudu na kuishi maisha bora na afya njema. Asasi ya SCF iliona kuna umuhimu wa kuwasaidia mashujaa wa saratani kumudu maisha yao mapya, eneo ambalo lilikuwa na upungufu katika nchi yetu.
“Kwa ujumla duniani kote idadi ya mashujaa imekuwa ikiongezeka kutokana na bidii ya uhamasishaji, elimu na maendeleo ya teknolojia katika tiba. Nasi SCF kutokana na uhusiano mzuri na Taasisi ya Kitafa ya Marekani ya iliyoasisi Maadhimisho ya Siku ya Mashuja wa Saratani (NCSDF) zaidi ya miaka 30 iliyopita, tumeona kuna umuhimu wa kuitambua na kuisheherekea siku hii nchini kwetu na mwaka huu ni wa nne.
Moja ya mambo ambayo SCF inayasisitizia katika maadhimisho haya ni kuielimisha jamii kwamba saratani hupona pale mtu anapobaini katika hatua za awali na kupata tiba sahihi. Wakati mwingine pia tiba ya saratani huwa ni ya muda mrefu na inayoandamana na madhila mengi ya kukatisha tamaa na ndiyo maana waliofanikiwa kupita vikwazo hivi wanapaswa kuitwa mashujaa.
“Tunaona huu ni muda muafaka kupitia siku hii mashujaa wa saratani kujuana, kufurahi na kupata uzoefu kutokana kwa wengine. Pia ni muda kwa mashujaa hawa kuwashukuru wale wanaowahudumia kama vile madaktari, wauguzi, familia na marafiki na hata taasisi zilizowahudumia. Hii ni sherehe baina yao wote kutokana na mafanikio yaliyopatikana.
“Watasheherekea na kupongezana kutokana na ukweli kwamba maisha ni zawadi ambayo tunapaswa kuina ni dhamana, yana kusudi na tunapaswa kumshukuru Mungu kwa uhai na afya njema.”

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD) katika Wizara ya Afya, Dkt. Omary Ubuguyu anasema Serikali inatambua changamoto ambazo watanzania wanakumbana nazo kuhusu afya na ndiyo maana imekuwa ikielekeza nguvu kubwa ya kuboresha huduma za afya nchini.

Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD) katika Wizara ya Afya, Dkt. Omary Ubuguyu

Anasema serikali imehakikisha hospitali zake zinakuna na vifaa vya kisasa vya uchunguzi, tiba, wauguzi, madaktari na hata wataalamu katika Nyanja zote.

Pamoja na juhudi hizo anasema changamoto hasa kwa wenye kipato cha chini zipo licha ya juhudi za kutoa misamaha kwa baadhi ya wagonjwa.”

Anasema Serikali inatambua hilo na ndiyo maana imekuwa ikitoa msamaha wa tiba kwa baadhi ya wagonjwa lakini msaada huo bado ni mdogo ukilinganisha na wahitaji.

Anasema wagonjwa wanaotibiwa kila mwaka ni 80,000 huku nusu yao ikiwa ni wapya hali ambayo imekuwa ikisababisha watoa huduma kufanya kazi hata baada ya muda wa kazi na mashine za huduma ya mionzi kuhudumia wagonjwa wanaokadiriwa kufikia 100 badala ya 30 kwa siku.

“Mfano mmemsikia Mkurugenzi (ORCI) akisema kila robo ya mwaka wanasamehe sh. bilioni saba ambazo ni sawa na karibu bilioni 30 kila mwaka,” anasema Dkt. Ubuguyu na kuitaka jamii kubuni mbinu za kusaidiana na serikali kutatua changamoto hizo.

Anatoa mfano kuwa watu wenye uwezo wajibidisha kuchangia huduma hizo kwa sababu kufanya hivyo kutaongeza uwezo wa taasisi kutoa msamaha kwa watu masikini.

Anaelezea kuwa jamii imekuwa ikionesha moyo wa kushirikiana kujenga makanisa na misikiti na kutoka moyo huo pia wautoe kwa ndugu wanaokabiliana na maradhi ya saratani.

Kwa upande wa Serikali, anasema wataendelea kuboresha hospitali za mikoa kama ilivyofanikiwa kwenye hospitali kuu za rufaa za kanda mfano KCMC mkoani Kilimajaro na Bugando mkoani Mwanza.

Dkt. Ubuguyu anataja mikakakti mingine ni asasi za kijamii pamoja na mashujaa wa saratani kuendelea kuwatia moyo wagonjwa na kuwasaidia kisaikolojia na maarifa ya kukabiliana na ugonjwa pamoja na matatizo mbalimbali ya ya kifamilia na kijamii.

Dkt. Ubuguyu anaitaka jamii na asasi kutafuta wahisani watakaowasaidia mashujaa kuwa na mitaji ya kuwawezesha kufanya ujasiriamali ili kupambana na tatizo la kipato wakati na baada ya kumaliza tiba.

Baadhi ya waliohudhuria maadhimisho haya wanaisifu asasi ya SCF kwa jinsi inavyowahamasisha na kuwaweka pamoja wagonjwa wa saratani na kuwapa moyo wa matumaini na kuwapa ushupavu wa kipekee wa kupambana na maisha.

Dk Harison Chuwa, kutoka hospitali ya Aghakan Tanzania, alielezea kuwa wagonjwa wengi wa saratani nchini wamekuwa wamekuwa wakiamini kuwa saratani siyo ugonjwa bali ni ushirikina.

Lakini asasi ya SCF imeleta mapinduzi ya kijamii kwa kuwezesha uelewa wa saratani kwa Watanzania na hata kuamini kwamba inaweza kutibika.