January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashirikisho, klabu za Karate mbioni kukutana

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MASHIRIKISHO pamoja na klabu mbalimbali za mchezo wa Karate zipo mbioni kukutana ili kutoa mapendekezo yatakayowasilishwa ndani ya Chama cha Shotokan Karate Tanzania (TASHOKA) yakatayosaidia katika maandalizi ya Kalenda ya mashindano kwa mwaka 2021.

Kikao hicho kinakwenda kufanyika baada ya kumalizika kwa mashindano ya Karate ya Afrika Mashariki ‘East African Shotokan Karate Championship’ yaliyomalidika wiki iliyopita hapa Dar es Salaam.

Katika mashindano hayo kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja ‘Individual’ mshindi wa Kata alitoka nchini Burundi huku kwa upande wa Kumite mshindi alitoka Dar es Salaam.

Kwa upande wa Wanawake Kumite mshindi alitoka Moshi na mshindi kwa upande wa Kata alitoka Dar es Salaam wakati kwa upande wa timu Dar ilishinda Kata na Kumite.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Mahusiano kwa Umma ya Shirikisho la mchezo wa Karate Tanzania (JKA/WF-TZ), Lawrence Mapunda amesema, kwa sasa kwa pamoja na mashirikisho wapo mbioni kukutana ili kushirikiana kutoa mapendekeza ambayo yataingia katika kalenda yao ya matukio ya mwaka ujao.

Kiongozi huyo amesema kuwa, lakini kabla ya kikao hicho cha pamoja wao kama JKA/WF-TZ wamekutana kwa ajili ya kufanya tathmini ya mambi mbalimbali ikiwemo mashindano yaliyofanyika kwa mwaka huu.

Lakini pia wapo kwenye mipango ya mwaka ujao kwani wataendesha semina kubwa mbili ambapo moja itafanyika kati kati ya mwaka na nyingine itafanyika mwishoni.

Itakumbukwa kuwa, mwanzoni mwa mwezi huu baada ya kumalizika kwa semina ya mchezo wa Karate ya Gasshuku 2020 iliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Desemba 4 Desemba 6, Songea Mkoani Ruvuma, viongozi mbalimbali walikubaliana kuwekeza nguvu zao katika mchezo huo ili kuhakikisha unasambaa katika Mikoa yote nchini.

Semina hiyo ambayo ujumbe wake mkuu ulikuwa ni kuhamasishana na kufanyia tathmini ya viwango vyao vya Karate ikiwemo kutengeneza ujirani mwema baina ya klabu moja na nyingine, ilishirikisha Makarateka zaidi ya 50 kutoka Dar es Salaam, Morogoro, Iringa pamoja na Wilaya za Masasi, Nachingwea, Nyasa pamoja na mashirikisho mengine ya Kimataifa ambayo yapo hapa nchini.

Kiongozi huyo alisema kuwa, tayari mwanga umeshaanza kuonekana kwani mafunzo hayo ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka yamekuwa na ongezeko kubwa la makarateka pamoja na kuongezeka kwa klabu.