Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WIZARA ya Maliasili na Utalii imesema Mashirika ya ndege ya Kimataifa ya Qatar Airways, Emirates na Turkish Airlines yanatumika kutangaza vivutio vya vivanvyopatikana nchini Tanzania.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Bungeni Mei 31,2024 na Waziri wa Wizara huyo ,Angellah Kairuki wakati akitaja vipaumbele vya wizara alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Vilevile amesema Wizara hiyo itaendelea kutangaza utalii ndani na nje ya nchi kupitia matangazo katika Ligi na Mashindano ya Michezo yenye wafuatiliaji wengi zaidi Duniani, kutumia watu mashuhuri na wenye ushawishi, Mabalozi wa hiari wa utalii, vyombo vya habari vya Kimataifa vyenye ushawishi pamoja na mitandao ya kimataifa ya utalii kama vile TripAdvisor na Expedia Group, vyombo vya habari kama CNN.
“Wizara itaendelea kukamilisha taratibu za kujitangaza kupitia Ligi za Michezo mikubwa Duniani za Marekani na Uingereza na Matukio makubwa ya Burudani,”amesema Kairuki.
Pia amesema Wizara hiyo itaweka mifumo maalum ya mawasiliano katika misitu ya hifadhi ya asili na mashamba ya miti ili kubaini matukio ya moto na kutoa elimu ya uhifadhi pamoja na kupambana na kuzuia matukio ya moto.
Aidha ameeleza kuwa katika kuelekea mkutano wa wadau wa Nyuki Kimataifa mwaka 2027 Wizara hiyo itaanza utekelezaji wa Programu ya Nyuki kwa Vijana na Wanawake ili kuandaa wataalamu na wajasilisamali wa mazao yatokanayo na asali na mazao mengine ya nyuki.
“Wizara itaandaa Miongozo na Taratibu za kutwaa na kuhamisha umiliki wa rasilimali za malikale kutoka kwa wamiliki kwenda kwa Wadau kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uhifadhi na kuandaa Mkakati wa utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Kale ya Mwaka 2008.
“Wizara itahuisha muda wa kulipa Ada ya Leseni ya Biashara za utalii na kuwa katika kipindi cha miezi 12 kuanzia siku ya mwisho ambayo wakala wa biashara za utalii amelipia leseni yake badala ya utaratibu wa sasa.
Hata hivyo amesema Wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha itapunguza Ada ya Leseni ya Biashara za utalii kwa wakala wa kupandisha watalii mlimani (mountain climbing), kufuta tozo kwa waongoza watalii wenye leseni hai kila wanapoingia hifadhini.
Kairuki alisema kuwa wadau watalipa ada ya Leseni ya Biashara za utalii kwa kutumia shilingi ya Tanzania badala ya Dola za Marekani pamoja na kuongeza muda wa Leseni ya Biashara za utalii kwa Waongoza watalii ambapo kwa sasa itadumu kwa kipindi cha miaka mitatu badala ya mwaka mmoja wa sasa.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba