Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MICHUANO ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za Msingi (UMITASHUMTA) na ile ya Shule za Sekondari (UMISSETA) ngazi ya Mkoa imezinduliwa jana katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa michuano hiyo Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alisema michezo hiyo ni muhimu sana kwani itawawezesha kukua kimwili na kiakili na pia itachochea ufundishaji, ujifunzaji na kuibua vipaji vyao.
Alibainisha kuwa michezo ni burudani, afya na ajira na pia huimarisha ushirikiano, upendo na undugu miongoni mwa wachezaji na kujenga vijana wenye nidhamu na uzalendo kwa taifa.
Aliongeza kuwa kupitia michuano hiyo baadhi yao watapata fursa ya kushiriki mashindano katika ngazi mbalimbali ikiwemo ya Afrika Mashariki na Kati (FEASSSA) hivyo kuwanufaisha zaidi.
Balozi Dkt.Batilda alisisitiza kuwa michuano hiyo ni sehemu ya utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo imeeleza bayana dhamira yake ya kutambua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi katika michezo mbalimbali.
Aliwataka waamuzi wa michuano hiyo na walimu watakaochagua timu za kuwakilisha Mkoa kutenda haki ili kupata timu bora itakayoleta ubingwa katika mashindano ya michuano ya ngazi ya taifa.
Afisa Elimu Mkoa Juma Kaponda alieleza kuwa wiki hii wanafanya mashindano ya UMITASHUMTA na wiki ijayo watafanya UMISSETA, wakimaliza wachezaji walioteuliwa kuunda timu ya Mkoa wataingia kambini moja kwa moja kujiandaa na mashindano ya taifa ambayo mwaka huu pia yanafanyikia Mkoani hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa ACP Richard Abwao aliwahakikishia wakazi wa Mkoa huo na wanamichezo wote kuwa ulinzi na usalama umeimarisha katika kipindi chote cha mashindano hayo hivyo wasiwe na wasiwasi.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM