October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashindano ya riadha, baiskeli kurindima Desemba 9

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online

MASHINDANO ya riadha na mbio za baiskeli ya kusheherekea Uhuru wa Tanganyika, yamepangwa kufanyika Desemba 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Kampuni ya Uhuru Sports Agency, Leena Kapadia amesema wanariadha wa kike na wa kiume watashindana kwenye mbio za Nusu Marathon kilomita 21, ambapo waendesha baiskeli watashindana mbio za Marathon kilomita 42.

Leena amesema mbali ya mashindano hayo, pia kutakuwa na mashindano ya kilomita tano ya kukimbia au kutembea, ambayo ni maalumu kwa watu wazima, vijana na watoto mbio za kilomita 10.

Amesema usajili wa washiriki katika mashindano hayo, utaanza Novemba 15 mwaka huu na Kamati yake kwa sasa inatafuta wadhamini kwa ajili ya kufanikisha tukio hilo muhimu, ambalo litakuwa la kwanza kufanyika nchini.

“Haya ni mashindano ya kwanza ya kusherehekea Uhuru wa Tanzania kwa kushirikisha wanariadha na waendesha baiskeli. Kampuni yetu imesajiliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kupata namba ya usajili ya NSC 83 na tunatarajia kufanya mbio zenye mvuto na ushindani mkubwa,” amesema.

Amesema pia wanakusudia kuona viongozi mbalimbali, makampuni ya umma, binafsi, mabalozi, taasisi kushiriki katika mbio hizo.

“Mfano, mbio za kilometa tano ni maalum kwa viongozi mbalimbali, familia na watu mbalimbali, wote hawa wanatakiwa kusheherekea Uhuru wa nchi yetu, hivyo tunawaomba wanamichezo kujisajili kwa ajili ya kushiriki katika mashindano haya,” amesema.

Amesema wanatarajia wanamichezo wasiopungua 3,500 kushiriki katika mashindano hayo, ambapo miongoni mwao ni wanariadha nyota wa ndani ya nchi.

Mkurugenzi huyo amesema mashindano hayo pia yana lengo la kuendeleza mchezo wa riadha na baiskeli hapa nchini.

“Hii ni fursa ya wanamichezo kujipima uwezo wao kabla ya kuwania nafasi ya kufuzu mashindano mbalimbali ya kimataifa,” amesema.