November 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashindano ya Gofu Lugalo kutimua vumbi Aprili 30,31

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

WACHEZAJI wa Kulipwa kutoka klabu mbalimbali za Gofu nchini wanatarajia kushiriki mashindano makubwa ya mchezo huo yatakayofanyika Aprili 30 na 31 katika viwanjwa vya Gofu vya Lugalo.

Katika mashindano hayo yanayofanyika kwa mujibu wa Kalenda, nyota wa kulipwa yatasindikizwa na wenzao zaidi ya 100 wa ridhaa ambao hadi sasa wameshajiandikisha kuwasindikiza wenzao

Akizungumza na Mtandao huu, Ofisa Habari wa Klabu ya Gofu Lugalo, Kapteni Selemani Semunyu amesema, hadi sasa nyota 25 wa kulipwa wameshathibitisha kushiriki michuano hiyo mikubwa ambayo mwaka huu yatakuwa ya kipekee kuwahi kutokea nchini.

Amesema kuwa, siku zote wachezaji wa kulipwa wamekuwa walimu wa wachezaji wa ridhaa hivyo wanatarajia kuona mchuano mkali na viwango vya hali ya juu ambavyo havioneshwi na wachezaji wa ridhaa.

“Lugalo tumeanza kutekeleza Kalenda yetu ya mwaka kwani Mwenyekiti wetu wa klabu, Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwogo anatamani kuona maendeleo makubwa sana katika Gofu na ndio maana mashindano haya yaana na wachezaji wa kulipwa ili wapate nafasi nzuri ya kukosoa yatakapokuja mashindano ya ridhaa,”.

“Hivyo Aprili 30 na 31 wachezaji wa kulipwa watapambana na tunategemea siku ya pili ya mashindano hayo tutapata wachezaji 10 Bora wa Kulipwa ambao watakwenda kupata zawadi na hadi sasa nyota 25 wameshathibitisha kushiriki,” amesema Kapteni Semunyu.

Kwa upande wake mchezaji wa kulipwa kutoka klabu ya gofu Lugalo, Frank Mwinuka amesema wamejipanga kikamilifu katika mashindano hayo kwani wanachokitaka ni kufanya vizuri ili kubakiza ubingwa nyumbani.

Koplo Lunacho Kigome ambaye ni mchezaji wa ridhaa kutoka klabu hiyo amesema, wamefanya mazoezi ya kutosha kujiimarisha ili kutoa upinzani mkali washiriki wengine ambao watachuana nao.