December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashindano kusaka bingwa wa Wavu Taifa kuanza Desemab 2

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MASHINDANO ya kumsaka bingwa wa Taifa wa mchezo wa Wavu kwa mwaka 2020 kwa upande wa wanaume na wanawake yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Desemba 2 hadi 6 mjini Morogoro.

Mashindano hayo yanakwenda kufanyika baada ya kupata mabingwa wa Mikoa ambao
ambao walianza kuchuana mwezi machi kabla ya serikali kusimamisha shughuli za michezo kutokana na mlipuko wa Corona

Kwa mujimu wa Kalenda ya TAVA iliyofanyiwa marekebisho mwezi Juni, awamu ya kwanza ya mashindano hayo ilianza Julai 4 hadi Agosti 22 huku ya pili ikianza Septemba 12 na kumalizika Novemba 21 ambapo sasa mshindi katika kila Mkoa atauwakilisha Mkoa wake katika mashindano hayo ya mchezo wa Wavu ya Taifa.

Kuelekea katika mashindano hayo tayari timu 13 za wanaume na saba za wanawake zimethibitisha ushiriki wao na sasa zipo katika maandalizi ya mwisho kabla ya wiki ijayo mashindano hayo kuanza.

Kwa upande wa wanaume timu ambazo zitashiriki hadi sasa ni
Jeshi Stars, JKT, Chui na UDSM VC zote za Dar es Salaam, Shinyanga VC, Moro Stars VC na Sua VC za Morogoro, Arusha Combine VC, Best Six VC na Must zitakazoiwakilisha Mbeya, MTC VC ya Mwanza , Dodoma Combine VC na Hazina zote za Dodoma.

Kwa upande wa timu za wanawake zipo Jeshi Stars, JKT, Stars Girls VC, Chui na Magereza VC zote za Dar es Salaam, Hazina VC ya Dodoma pamoja na Mkalapa Girls ya Mtwara ambapo bingwa wa mashindano hayo ataondoka na kitita cha Sh. milioni 2, mshindi wa pili atazawadiwa milioni 1 huku Laki 5 zikienda kwa mshindi wa tatu.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mpira wa wavu Tanzania (TAVA) Alfred Selengia ambaye pia ni Mkufunzi wa kwanza wa makocha wa mpira wa Wavu na Wavu Ufukweni kutoka Tanzania na Afrika kwa ujumla ameuambia Mtandao huu kuwa, licha timu hizo 20 kuthibitisha ushiriki wao lakini huenda kukawa na ongezeko la timu.

“Tunatarajia kuwa na ongezeko la timu kwa siku hizi zilizobaki kwani bado kuna mabingwa ambao hawajathibitisha ushiriki wao hadi sasa kutokana na kutokaa vizuri kiuchumi hivyo hadi mwisho wa wiki tutakuwa tumepata idadi kamili wa timu zitakazoshiriki, ” amesema Selengia.

Hata hivyo ameweka wazi kuwa, kutokana na jinsi mambo yalivyo watahakikisha wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha mchezo huo unachezwa nchi nzima na wamejipanga ndani ya miaka mitano ijayo kuwe kuna ongezeko kubwa la idadi ya timu pamoja na kuhamasisha kuundwa kwa klabu mbalimbali.