December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashabiki wa Yanga waadhimisha wiki ya wananchi kwa kuwagusa wahitaji

Na Lubango Mleka, Times Majira Online Igunga.

WANACHAMA na mashabiki wa timu ya Yanga Wilaya ya Igunga mkoani Tabora wameadhimisha wiki ya Mwananchi kwa kutembelea wodi ya watoto hospitali ya Wilaya hiyo pamoja na wafungwa wa Gereza Kuu wilayani humo na kutoa mahitaji mbalimbali.

Kilele hicho kimeanza kwa maandamano ya amani kutokea uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine uliopo Mamlaka ya Mji mdogo wa Igunga na kuelekea Hospitali ya wilaya ya Igunga ambapo wamewafariji Wazazi na watoto ambao ni wagonjwa kwa kuwapatia juisi, maji ya kunywa, sabuni za unga na vipande, dawa za meno, mafuta pamoja na pampasi.

Wamehitimisha maadhimisho hayo kwa kutembelea Gereza Kuu Wilaya ya Igunga ambapo wametoa kiasi cha sh. 30,000 kwa ajili ya kununua kifurushi cha Azam ili wafungwa na mahabusu wapete fursa ya kufuatilia kilele cha wiki ya Mwananchi,.

Mbali na hiyo wametoa sabuni za unga na vipande, viwembe, maji ya kunywa na mipira miwili kwa ajili ya wafungwa na mahabusu kufanya mazoezi.

Mkaguzi Msaidizi I. R. Ntandu kwa niaba ya Mkuu wa Gereza hilo amewashukuru wanayanga hao kwa kuguswa na kukumbuka kuwa kuna watu ambao ni miongoni mwa jamii wanaohitaji faraja kwa kuwapatia mahitaji muhimu.

Mmoja ya wazazi ambaye mtoto wake amelazwa katika hospitali hiyo Jackline Dickson amesema walichofanya wanayanga hao ni zaidi ya timu na hiyo ni neema ya kipekee kwao hivyo amewaomba waendelee kufanya makubwa.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Lucia Kafumu, Muuguzi Msaidizi Nyasatu Daniel amewaomba kujitoa zaidi kwa kurudisha fadhila kwa jamii kwani michezo ni amani na furaha hivyo wameonesha furaha kwa wazazi na watoto wao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tawi la Yanga Bingwa Igunga Mjini Paul Mtani amesema kuwa wamewatembelea watoto,wafungwa na mahabusu kwani ndio kundi ambalo wameona linauhitaji mkubwa.