November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Masauni atoa agizo kali wanaotumia vibaya uhuru wa maoni

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mhandisi Hamad Masauni ametoa onyo kali kwa watu wanaotumia uhuru wa kutoa maoni vibaya kwa lengo la kuhatarisha usalama na kuleta mpasuko kwa taifa.

Kauli hiyo imekuja baada ya kuibuka baadhi ya watu hususani wanasiasa kutumia majukwaa yao kutoa kauli zenye viashiria vya uvunjifu wa amani vyenye kuleta mgawanyiko nchini.

Masauni alitoa tamko hilo wakati akizungumza na wananchama wa Chama Cha Mapinduzi Kinondoni ambapo aliwataka kutumia uhuru wa kutoa maoni kwa maslahi ya Taifa huku wakidumisha uhuru na mshikamano.

“Katika nchi hii kama kuna chama kinachosifika katika ujenzi na misingi ya umoja na mshikamano ni Chama Cha Mapinduzi(CCM) na ndicho kina dhamana ya kuiongoza serikali ambayo ina jukumu la kuhakikisha nchi inabaki kuwa salama kudumisha umoja na mshikamano, vyama vingine havina jukumu hilo.”

Alisema CCM kina dhamana ya kudumisha misingi ya umoja na mshikamano, udugu na hatimaye kisababisha usalama. Masauni alisema anafarijika kuona wanachama wa CCM wenzake wa Kinondoni na jimbo la Kikwajuni kuwa wajumbe wazuri hususani kwa vijana kuimarisha muungano.

“Sote tumeshuhudia juu ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo na ustawi nchini na jambo kubwa linaloendelea kuipa heshima Tanzania ni uamuzi wake wa kuimarisha diplomasia ya uchumi, demokrasia na uhuru wa kujieleza.”

Alisema dhamira ya Rais Dk.Samia ni njema kwa sababu Chama kinafungua milango ya mawazo na ushauri kutoka kwa mtu yeyote kwa sababu nchi hii ni ya watu.

“Tutaendelea kupokea ushauri, mawazo na maoni lakini bahati mbaya kumekuwa na baadhi ya Watanzania wenzetu wamekuwa wakitaka kuanza kutumia uhuru huo vibaya kiasi cha kutoa kauli ambazo zinalenga kuhatarisha usalama wa nchi, kuvunja sheria za nchi hii na kulipasua taifa, “alisema.

Masauni alisema kauli hizo haziwezi kuvumika kwani haiwezekani kutumia kisingizio cha uhuru kutoa maoni kuvunja sheria za nchi.Aliwataka wanachi kujiepusha kutumia uhuru huo uliotolewa kwa nia njema katika kuvunja sheria za nchi.

“Ninalielekeza jeshi la polisi na vyombo vingime vya usalama kuhakikisha havimfumbii macho mtu yeyote au kikundi chochote kitakachopelekea kwa vitendo au kwa kauli katika kuvunja sheria za nchi yetu na kuhatarisha usalama wa nchi hii, ” alisema.

Masauni alisema anaamini kasi ya maendeleo kwa serikali kwa muda mfupi imetokana na dhamira ya dhati ya Rais Dk.Samia na hatua alizozichukua katika kukuza uwekezaji kupitia sekta binafsi, biashara kuimarika na mahusiano yabkimataifa ja kuwezesha kuoa fedha nyingi za masharti nafuu kwa maendeleo ya wananchi.