Na Esther Macha, Timesmajira Online,
MBUNGE wa Jimbo la Lupa wilayani Chunya mkoani Mbeya Masache Kasaka amesema pamoja na uzalishaji mkubwa wa nishati ya umeme bado nguvu kubwa inahitajika katika usambazaji pamoja na usafirishaji ili wananchi waweze kupata nishati hiyo kwa uhakika .
Masache amesema hayo Aprili 25 ,2024 wakati akichangia hoja ya Wizara ya Nishati katika kikao cha Bunge kinachoendelea jijini Dodoma.
“Tulipita kipindi kigumu hapa katikati cha changamoto ya umeme lakini kwa ushirikiano mkubwa kazi ilifanyika pamoja na uzalishaji huu bado kunahitajika nguvu ya kuelekeza kwenye uzalishaji na usambazaji,”amesema.
Amesema kwa sasa wanataka kuona umeme unapatikana wanapo waambia wananchi uzalishaji upo wa kutosha na ziada lakini wakiona baadhi ya maeneo umeme unakatika wanakuwa hawawaelewi kabisa.
Hata hivyo Kasaka ameiomba Wizara ya Nishati kutenga fedha na bajeti ya kutosha kwenye usafirishaji na usambazaji ili wananchi waweze kunufaika na umeme wa uhakika.
“Naungana naWabunge wenzangu kumpongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Dotto Biteko pamoja na watalaamu wengine wa Wizara hii kwani wanafanya kazi kubwa na tunaiona jinsi ilivyopambana kwenye suala la umeme ambalo lilikuwa changamoto kubwa kwa wananchi,”amesema Mbunge Kasaka.
Aidha Kasaka amepongeza Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kwani wamekuwa wakifanya kazi kubwa na kuomba kuongeza nguvu ili wananchi ambao vijiji vyao havijapitiwa na umeme viweze kufikia na nishati hiyo.
Amesema Wilaya ya Chunya kuna changamoto ya umeme kuna vijiji havijafikiwa na nishati hiyo katika Kata tatu ikiwemo Luaraje ambayo ina vijiji viwili na tayari miundombinu yake ipo tayari lakini haujawafikia wananchi wa vijiji hivyo.
Amesema wakati mradi huo unapelekwa Kata ya Luaraje hakukuwa na shule ya Sekondari lakini sasa ipo hivyo ameiomba Wizara ya Nishati na Rea kuifikishia umeme ili iweze kunufaika wakati mkandarasi akiwa bado yupo eneo la kazi ili wananchi waweze kunufaika.
Pia amesema Kata ya Mafyeko na Kambikatoto hazijafikiwa na umeme kwasababu mkandarasi aliyekuwepo alipata changamoto na mkataba kusitishiwa.
“Pamoja na umeme kwenda kwenye vijiji hivyo Wilaya ya Chunya kuna mradi wa kupeleka umeme kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo na kusema mradi upo kwenye asilimia 28 mpaka 30.”amesema na kuongeza kuwa
“Naiomba serikali kupeleka fedha za kutosha kuwafikia wachimbaji na wao waweze kunufaika na uzalishaji wa madini ya dhahabu uweze kufanyika na kuongeza Pato la Taifa.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa