Esther Macha, TimesMajira Online, Mbarali
MKAZI wa Kijiji cha Majengo Kata ya Igurusi Wilayani Mbarali, Mbeya, Mary Mwaipopo (50) amewataka watu wenye ulemavu kujishughulisha kwa kufanya shughuli za ujasiriamali mdogo ili waweze kulea familia zao kwani ulemavu sio sababu ya kukaa na kusubiri kupewa au kuomba kama wanavyofanya wengi.
Akizungumza na Mtandao huu, Mary amesema kuwa baadhi ya watu wenye ulemavu wamekuwa wakitumia ulemavu wao kama sehemu ya kubweteka na kutofanya shughuli yeyote kwa kuona kuwa ulemavu walionao unawakwamisha kufanya shughuli yeyote ya uzalishaji mali.
Mlemavu huyo amelisema ni lazima ifike wakati walemavu wengine waache tabia ya kuomba omba mitaani au kukaa barabarani na badala yake wajishughulishe kwa kufanya ujasiliamali wa aina mbali mbali kulingana na mahitaji ya sehelu walizo.
Amesema kuwa, kujishughulisha kutawafanya kuondokana na hali ya kuwa omba omba ambayo hivi sasa imeota mizizi kwa baadhi ya walemavu ambao wanaona kwa hali walizonazo hawawezi kufanya shughuli yeyote zaidi ya kuomba.
“Mimi hapa nilipo toka nikiwa na miaka mitatu sijawahi kutembea ni kutambaa lakini bado hii hali nilinayo sitaki kukaa barabarani na kuwa omba omba, hivi nilivyo nafanya biashara zangu ndogo ndogo pamoja na kushona maturubai na kushona nguo za watoto kwa kutumia chelehani yenye kitako ambayo inaniwezesha kufanya kazi zangu vizuri za kupata fedha kidogo za kuendeshea maisha yangu na familia,” amesema Mary.
Akimzungumzia Mary, mmoja wa wakazi wa kijiji cha Muungano Kata ya Igurusi, Shukuru Juma amesema, licha ya ulemavu alionao lakini amekuwa akifanya shughuli mbali mbali ikiwemo kushona maturubai kipindi cha mavuno ya mpunga, kupinga kanga, kuweka viraka nguo za watoto zilizochanika .
“Binafsi mimi huwa napata imani sana kwa mama huyu napita apa kwake kumsaidia chochote ninachokuwa nacho maana katika jamii tuna walemavu wengi wamekaa tu sasa huyu mama anajituma hivyo unapata moyo wa kumsaidia ,”.
“Kupitia shughuli zake mama huyu ameanza ujenzi wa nyumba yake ambayo ikikamilika atahamia na familia yake. Ndugu mwandishi huyu mama alikuwa na watoto sita lakini mpaka sasa kabaki na mtoto mmoja tu ambaye ana umri wa miaka (21)ambaye kiuhalisia naye hana msaada na Mume wake wake alifariki hivyo maisha yake ni duni kwa ulemavu alionao anahitaji kusaidiwa hata kupata mtaji auze nyanya,” amesema Shukuru.
Diwani wa Kata ya Igurusi, Hawa Kihwele amesema kuwa katika hiyo kuna baadhi ya walemavu ambao aliwasaidia vyerehani ya kushonea nguo ambapo mmoja wapo ni Mary Mwaipopo ambayo mpaka hivi sasa anaendelea kuitumia katika shughuli zake za ushonaji.
“Naendelea kutafuta wadau wengine katika maeneo mbalimbali ili tuweze kuwasaidia walemavu waliopo katika kata hii akiwemo mama Mary ambaye kutokana na ulemavu wake hatembei ni mtu wa kutambaa,” amesema Diwani huyo.
More Stories
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania