January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maroboti yageuka kivutio Sabasaba

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

BAADHI ya wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wameshauri Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE),kuongeza siku za maonesho
kutokana na kuongezeka kwa burudani katika maonesho hayo ikiwemo maroboti.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti ndani ya maonesho hayo ya 48 ya Biashara Kimataifa maarufu kama Sabasaba, Valentino Kivike amesema maonesho hayo,serikali ingeangalia namna ya kuongeza siku ili watu waweze kujionea vivutio mbalimbali ikiwemo Maroboti yaliyomo ndani ya viwanja vya Sabasaba.

Amesema maonesho ya mwaka huu yamekuwa tofauti na miaka ya nyuma kutokana na serikali kuboresha miundombinu yake pamoja na kuwepo kwa mabanda mengi zaidi.

“Sijawahi kuona hii ni teknolojia mpya,na hii ni mara ya kwanza kwa maonesho haya kuweka maroboti haya ambayo yanaweza kufaa hata kazi na mambo mengine,”amesema na kuongeza

“Watu wajitokeze tu ,kuja kuona vivutio hivi,kwa mara yangu ya kwanza mie kuona roboto kwa macho yangu ,tumefurahi tumeweza kupiga picha nayo na hata kupiga nayo story, “amesema.

Kwa upande wake ,Amina Said Mkazi wa Mbagala amesema kwa mara ya kwanza yeye amemuona roboto na kupiga nae picha hii imekuwa kama bahati kwake.

Amesema mbali na kivutio hicho pia amefurahi kuona wajasiriamali mbalimbali pamoja na mabanda ya taasisi za serikali katika maonesho hayo ambayo yamekuwa yakiwasaidia kujua mambo mbalimbali ya wanayoyafanya.

“Unajua kuna watu hawaji Sabasaba kwa sababu wanahisi hakuna kitu kipya chakujifunza lakini wanapaswa kujua kuwa ukija huku utapata burudani ,unatengeneza afya ya akili,”amesema.

Amesema ni wakati serikali kutoa nafasi zaidi kwa wabunifu wa stadi za mikono na bunifu nyingine.

Maonesho ya Sabasaba yalianza rasmi Juni 28 na yatarajiwa kumalizika Julai 13.