November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Marekani kuipatia Tanzania mabilioni ya fedha

Na Mwandishi Wetu

MAREKANI kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) itaongeza Tanzania kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 2.4 (Takriban sh. bilioni 5.6), ikiwa ni msaada wake kwa sekta ya afya nchini.

Msaada huu unalenga kuimarisha uwezo wa maabara na upimaji wa kimaabara, kusaidia jitihada za utoaji taarifa (risk communication), miradi ya maji na usafi wa mazingira na kuzuia na kudhibiti maambukizi.

Maeneo mengine ni ya kutoa elimu ya afya kwa umma na miradi mingine. Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolea leo, fedha hizo ni nyongeza ya msaada wa Dola za Kimarekani milioni 1 unaolenga kusaidia mapambano dhidi ya janga la COVID-19 uliotolewa hivi karibuni na kufanya kiasi kipya cha fedha zilizotolewa kwa Tanzania kukabiliana na janga hilo kufikia Dola za Kimarekani milioni 3.4.

Isitoshe, kiasi kingine cha Dola za Kimarekani milioni 1.9 zimebadilishwa matumizi na kuelekezwa kwenye mapambano dhidi ya janga hili.

Hii inafanya jumla ya fedha zote zilizotolewa na Marekani katika kukabiliana na COVID-19 nchini Tanzania hadi hivi sasa kufikia Dola za Kimarekani milioni 5.3 (sawa na sh.bilioni 12.2).