Na Joyce Kasiki Timesmajira online Dodoma
KATIBU Mkuu mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Asha-Rose Migiro, amemshukuru kwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinfuzi (CCM ) na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini kuona kwamba anaweza kuvaa viatu vya aliyekuwa Katibu mkuu wa CCM Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi na kushika wadhifa huo.
Akizungumza mara baada ya kupokelewa katika Ofisi za CCM Makao Makuu ambapo alipokelewa na mamia ya wanachama mkoani huo Dkt. Migiro alisema uteuzi huo ni heshima kubwa na dhamana ya kuendeleza misingi imara ya uongozi wa chama hicho tawala, huku akiahidi kulitumikia kwa uadilifu, bidii na uaminifu.
“Ninatoa shukrani za dhati kwa Mwenyekiti wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuniamini na kunikabidhi jukumu hili kubwa. Ni heshima kubwa kwangu, na naahidi kulitumikia chama chetu kwa moyo wangu wote, kwa weledi na kwa maslahi mapana ya Taifa,” amesema Dkt. Migiro.
Aidha, amewataka wanachama wa CCM kuendelea kushikamana kwa lengo la kuhakikisha ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Aidha, Dkt. Migiro pia amewashukuru wanachama kwa mapokezi mazuri, akisema kuwa ni ishara ya mshikamano, umoja na mapenzi ya dhati yaliyokita mizizi ndani ya CCM.
Kwa upande wake Balozi Dkt.Nchimbi, alimwelezea Dkt.Migiro kuwa ni kiongozi mwenye maono, uzoefu mkubwa na rekodi ya mafanikio katika nyanja mbalimbali za utumishi wa umma, kitaifa na kimataifa.
“Ninampongeza dada yangu, Dkt. Migiro, kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM. Ana uzoefu mkubwa wa kiuongozi na anastahili nafasi hii. Namuombea mafanikio mema katika kulitumikia chama chetu,” amesema Dkt. Nchimbi.
Aidha, alitoa shukrani kwa Mwenyekiti wa CCM kwa kumuamini katika kipindi alichokihudumia chama kama Katibu Mkuu, na kuwashukuru wanachama wote kwa ushirikiano waliomuonyesha.
“Nilijiunga na chama hiki nikiwa kijana mdogo, nimetumikia nyadhifa mbalimbali ndani ya serikali na chama, na naondoka nikiwa na imani kubwa kuwa CCM iko katika mikono salama,” aliongeza Dkt. Nchimbi.
Uteuzi wa Dkt. Migiro umeweka historia mpya ndani ya CCM tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977 kufuatia muungano wa vyama vya TANU na Afro-Shirazi Party (ASP), kwa kuwa ni mara ya kwanza mwanamke kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Katika kipindi cha miaka 48 ya uhai wa CCM, nafasi hiyo ilikuwa imeshikiliwa na viongozi wanaume pekee, kuanzia Mzee Pius Msekwa hadi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ambaye sasa ni mgombea mwenza wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
DKT. MIGIRO: KIONGOZI MWANADIPLOMASIA WA KIMATAIFA
Dkt. Migiro ni mwanazuoni mwenye historia pana ya uongozi, akiwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kati ya mwaka 2007 na 2012, baada ya kuteuliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja huo, Ban Ki-Moon.
Kabla ya hapo, alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete. Dkt. Migiro pia amewahi kuwa mhadhiri wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka 2016, aliteuliwa na Rais Hayati John Pombe Magufuli kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza ,nafasi ambayo ilimpa fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika moja ya nchi muhimu duniani, hasa kwa kuzingatia historia ya Uingereza kama mtawala wa kikoloni wa Tanganyika kabla ya uhuru mwaka 1961.
Kwa uteuzi huu, Dkt. Migiro anabeba matumaini mapya ya uongozi wa kisasa ndani ya CCM, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, na pia anaimarisha nafasi ya wanawake katika siasa za juu nchini Tanzania.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina