November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari kufikishwa Bungeni Januari

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile, amesema mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari yatafikishwa bungeni Januari 2023.

Hayo ameyasema leo wakati akizungumza katika Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 lililofanyika katika ukumbi wa mikutano JNICC jijini Dar es Salaam

“Nimezungumza na Waziri Nape (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) kuhusu mjadala wa Sheria ya Huduma za Habari, amesema Januari (2022) mapendekezo yatafikishwa bungeni,” amesema.

Balile amesema, wadau wa habari nchini wanafurahia uhuru uliopo lakini haujalindwa kisheria.

“licha ya kuwepo kwa uhuru wa habari nchini, ameomba uhuru huo ulindwe kisheria.”

“Wadau wa habari nchini wanafurahia uhuru wa habari uliopo nchini, tunaamini serikali italinda uhuru huu kisheria katika Mabadiliko ya Sheria ya Habari yajayo.” Ameongeza Balile

Akizungumzia madeni ya vyombo vya habari katika serikali na taasisi zake, Balile amesema licha ya juhudi kufanywa, bado taasisi za serikali ikiwemo halmashauri hasijalipa madeni yao kwa vyombo vya habari.

“Mpaka mwishoni mwa mwaka jana, madeni ambayo vyombo vya habari vinadai kwa serikali na taasisi zake ni Tsh. 7 bilioni.

“Ukijumuisha na deni la Gazeti la Daily News la serikali (Tsh. 11 Bilioni), jumla ya deni ni Tsh. 18 Bilioni na zaidi,” amesema.

“Halmashauri wana roho ngumu, hawajalipa mpaka leo licha ya kuandikiwa barua na TAMISEMI. Tunaomba mheshimiwa waziri (Nape) liwekee mguu chini, utusaidie,” amesema Balile.

Katika mapendekezo ya mabadiliko ya sheria, miongoni mwa mapendekezo ya wadau wa habari, ni kuweka sheria itakayowalazimisha watangazaji kwenye vyombo vya habari kulipa fedha ndani ya miezi sita baada ya matangazo yao kuchapishwa.

Miongoni mwa adhabu iliyopendekezwa iwapo mtangazaji atashindwa kulipa, walau kifungo cha miezi Sita.