January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mapendekezo ya ACT Wazalendo kwa Serikali

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Chama cha ACT Wazalendo wameiomba Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi yakayowezesha kuwepo kwa ongezeko la ajira kwa vijana ili kwenda kuimarisha huduma za elimu, afya na kilimo na
maeneo mengine yenye uhitaji.

imeelezwa kuwa ukosefu wa ajira hupelekea kuongezeka kwa wimbi
la umasikini na utegemezi, kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili na uhalifu nchini ikiwemo
vitendo vya wizi, ukahaba, unyang’anyi, uporaji pia kuongezeka kwa upendeleo, kujuana, rushwa
katika utolewaji wa kazi, kuongezeka kwa utumikishaji wa watoto kwa ujira mdogo au bila malipo
hususani; mashuleni, viwandani, majumbani, migodini nk kwa kigezo cha kupatiwa ajira.

Hayo aliyasema Waziri Mkuu Kivuli ACT Wazalendo Dorothy Semu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuhusu Mapitio ya kazi na mwelekeo wa Serikali na
makadirio ya matumizi kwa Mwaka wa Fedha wa 2023/2024.

“Ofisi ya Waziri Mkuu inahusika moja kwa moja na masuala ya ajira na uwezeshaji kupitia Wizara
ya Vijana, kazi na ajira. Mwenendo na hali ya ukosefu wa ajira nchini inazidi kuwa tata sana,
uchumi wetu unazidi kupunguza uwezekano wa kuzalishaji ajira zenye staha na shughuli za
kueleweka za kuwapatia vijana vipato ili kumudu maisha yao. Takwimu zinaonyesha ukweli kwa
namna tofauti tofauti.”

Aidha ACT Wazalendo waliiomba Serikali kununua na kuhifadhi chakula cha kutosha angalau miezi
3 kutokana na chakula kitachovunwa mwaka huu ili kujilinda na upungufu wa chakula.

Aidha waliiomba Serikali iweke mazingira bora kwa wakulima wadogo ili kuongeza uzalishaji zaidi; kwa
kuendelea kutoa ruzuku katika mbolea na kusimamia usambazaji wake; kuhakikisha usalama
wa ardhi kwa Wakulima wadogo kwa kushughulikia migogoro ya ardhi.

“Kutokana
na ukweli kuwa kwa maeneo mengi nchini uzalishaji unaweza kuwa sio mzuri kwa mwaka huu.
Hatua hii itawezakana kwa Serikali kujenga uwezo wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
(NFRA) kwa kutenga bajeti ya kutosha ya kununua chakula (Tani Milioni 1.5 za Mahindi, Tani
laki 5 za Mpunga, Maharagwe tani Milioni 1). Aidha, kuwezeshwa Bodi ya mazao mchanganyiko
kununua na kusambaza chakula kwenye eneo linaloonyesha uhaba/upungufu wa chakula.”

Mbali na hayo ACT wameiomba Serikali kuwalipa fidia stahiki wananchi waliohamishwa ngorongoro kwani kuna uharibifu walioufanya na
kuwahamisha makazi yao bila matakwa yao ambayo imepelekea kukwamisha shughuli zao za
kimaendeleo pia wengine kupoteza baadhi ya mali zao.

Mbali na hayo, ACT wameiomba Serikali kuja na Sera mpya ya fidia kwa wananchi
wanaopisha maeneo ya uwekezaji, Sera itakayobeba utaratibu wa ardhi kwa uwekezaji (Land
for Equity) uanze kutumika katika miradi yote nchini ambapo ardhi ya wananchi itumike kama
mtaji katika mradi na hivyo kuzipa Serikali za mitaa za maeneo husika umiliki katika miradi.

Pia ACT walisema Wananchi wajengewe makazi mbadala maeneo yaliyopimwa na yenye huduma zote za kijamii
na vile vile wapewe shughuli mbadala za kiuchumi kama vile ufugaji wa samaki, ufugaji wa kuku,
kilimo.