Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza
Katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha wa 2024/2025(Januari-Machi,2025) Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imefikia na kutekeleza miradi zaidi ya 50,ya sekta mbalimbali ikiwemo ile ya kuendeleza ili ikamilike.
Ambapo katika kipindi hicho zaidi ya milioni 834 fedha za mapato ya ndani zilielekezwa kwenye miradi hiyo ya maendeleo ikiwa ni utekelezajia wa bajeti ya mwaka 2024/2025.

Hayo yameelezwa Aprili 11,2025, na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Ummy Wayayu,wakati akiwasilisha taarifa yake kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hili kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Ummy amesema,miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na sekta ya ujenzi,mipango miji na miundombinu ambapo zilielekezwa zaidi ya milioni 280,sekta ya elimu msingi milioni 212.5 na elimu sekondari zaidi ya milioni 92.

Huku sekta ya afya milioni 80,maendeleo ya jamii zaidi ya milioni 69,utawala zaidi milioni 24,usafi wa mazingira na udhibiti wa taka ngumu milioni 5,sekta ya kilimo,biashara na uwekezaji zaidi ya milioni 39.
Diwani wa Kata ya Buswelu,Sarah Ng’hwani,amesema katika robo hiyo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2024,Kata yake imefikiwa na miradi mingi ikiwemo ya elimu ambapo alipata kiasi cha milioni nane kwa ajili ya ujenzi wa choo cha matundu 10, na milioni 12 kwa ajili ya kukamilisha madarasa matatu shule ya msingi Bujigwa.
Amesema,vikundi sita kutoka kata hiyo vilipata fedha za mkopo wa asilimia 10 za Halmashauri kati yao mlemavu mmoja aliepatiwa bajaji,kikundi cha vijana wamepata bajaji za mizigo 6 na vikundi 4,ni vya wanawake huku ujenzi wa barabara mbili za kiwango cha lami ukiendelea.
Kwa upande wake Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Manusura Lusigaliye,amesema ndani ya miaka mitano Kata ya Buzuruga imepokea jumla ya kiasi cha bilioni 3.7,kutoka Serikali Kuu na mapato ya ndani na kuifanya kata hiyo kupiga hatua katika sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu,barabara na afya.

More Stories
Polisi kuchunguza madai ya mwanafunzi kutupa kichanga chooni
Sekiboko ahimiza uwekezaji Elimu ya ufundi
Wazee wawili jela maisha kwa kubaka na kulawiti