Ashura Jumapili, TimesMajira Online, Kagera
Waandishi wa habari ,mkoani Kagera wametakiwa kuendelea kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa Marburg,ili iwe na uelewa na kuweza kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.
Wito huo umetolewa Januari 28,2025, na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajath Fatima Mwassa,mjini Bukoba wakati akifungua mafunzo kwa Waaandishi wa habari kutoka wilaya zote za Mkoa huo yaliotolewa na Wizara ya Afya kwa kushirikina na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF).
Amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa kuhusu ugonjwa wa Marburg na umuhimu wa kutoa taarifa sahihi ambazo siyo za kuleta taharuki katika jamii.
“Busara ya habari ni kutoa taarifa sahihi na sio kutoa taarifa zenye upotoshaji za kuleta taharuki, hivyo nitoe wito kwa wanahabari tutoe elimu na taarifa kwa usahihi,muwe mabalozi katika kupambana na ugonjwa wa Marburg, watu wasirundikane kwenye misiba, kwenye sherehe,”amesema Mwassa.
Huku akiwahimiza wanahabari kuepuka kutumiwa kuwa wachochezi na badala yake kutoa elimu kuhusu ugonjwa wa Marburg, unavyoenea, dalili zake na jinsi ya kujikinga nao.
“Wanahabari lazima tupambane kushirikiana kudhibiti ugonjwa huo,tunapozungumzia kuzuia maambukizi mfano kunawa mikono kwa maji tiririka, hatuzuii marburg pekee, tunazuia pia na magonjwa mengine ya mlipuko kama vile mpox na kipindupindu,”amesema.
Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ntuli Kapologwe,amesema mafunzo hayo kwa wanahabari yatasaidia kuondoa habari zinazopotosha jamii .
“Ninyi ni muhimu,mtachochea mabadiliko chanya kwa jamii kuondokana na imani potofu kuhusu ugonjwa wa marburg,”amesema.
Mratibu wa huduma za afya ngazi ya jamii kutoka Wizara ya Afya Dkt. Norman Jonas,amesema ugonjwa wa marburg husababishwa na virusi na unasambaa kwa njia kuu mbili ambazo kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu kwa kugusa majimaji.
Pia amezitaja baadhi ya dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa kali, kutokwa damu sehemu za wazi za mwili kama vile, puani, masikioni, kutapika damu na kuharisha.
Mwakilishi kutoka Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani(UNICEF) Dkt. Edna Moturi,amesema kwa kushirikiana na Serikali wataendeleza mafunzo kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo wahudumu wa afya ngazi ya jamii, waganga wa tiba asili, bodaboda na makundi mengine.
Nao Baadhi ya wanahabari walionufaika na mafunzo hayo akiwemo Benson Eustace, wamesema,mafunzo hayo yatasaidia kuandika habari zilizo sahihi na zenye kuelimimisha badala ya kuleta taharuki katika jamii.
More Stories
Serikali kuchukua hatua madhubuti kuboresha ufaulu masomo ya sayansi
Wasira:Gari ni injini siyo bodi
HGWT yapongezwa kuwapa hifadhi wasichana