Na Mwandishi Wetu, Timesmajira OOnline
SERIKALI imewaalika wananchi na wadau mbalimbali kuhudhuria mkutano wa kukusanya maoni kuhusu Sera mpya ya biashara ndogo ndogo (SMEs) utakaofanyika mkoani Dodoma .
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. John Simbachawene, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa siku ya viwanda vidogo vidogo (TAMISID).
Siku ya viwanda vidogo vidogo inayotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu mkoani Dodoma inaratibiwa na Chama cha Wenye Viwanda Vidogo Tanzania Association of Small Scale Industries and Manufacturers (TASSIM).
Alisema serikali ilikusanya maoni ya watu mbalimbali kwenye awamu ya kwanza hivyo imeamua kuandaa mkutano wa awamu ya pili kuchukua maoni kwa wale ambao walikosa nafasi kwenye awamu ya kwanza.
Alisema mkutano huo utafanyika wiki hii mkoani Dodoma na kuwataka wananchi, wajasiriamali, wafanyabiashara kushiriki kwenye mkutano huo ili watoe maoni ya kuchangia kuboresha sera hiyo.
“Wizara inaendelea kuifanyia kazi Sera mpya ya viwanda na tumeitisha mkutano wa wadau mbalimbali mkoani Dodoma waje kutoa maoni yao kwa awamu ya pili kwa ambao hawakutoa maoni yao ili tukamilishe hiyo Sera na iweze kutoa mchango wake kwenye taifa letu na tuweze kuizindua rasmi,” alisema Dk. Simbachawene
Alisema malengo makuu ya siku ya viwanda vidogo ni pamoja na kuongeza uelewa wa mchanago wa viwanda vidogo katika uchumi na kukuza ubunifu kwenye sekta.
”Kama tulivyoona wakati tunatembelea maonyesho zipo bidhaa ambazo zimetengenezwa na wajasiriamali wadogo ambazo ni bora na zinaweza kushindana kimataifa kwa hiyo nawasisitiza wajasiriamali waendelee kuwa wabunifu wa bidhaa,” alisema
Aidha, alisema kuanzishwa kwa taasisi hiyo kutakuwa ni jukwaaa la kuwaunganisha wadau wawekezaji na washirika wa maendeleo katika kuendeleza viwanda vidogo na kuwajengea uwezo kupitia mafunzo.
Alisema TASIM inafanya maandalizi ya maonyesho ya viwanda vidogo Tanzania yatakayofanyika tarehe 28 Oktoba hadi Novemba Mosi kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma na kuwataka wajasiriamali kuitumia kama fusa kwao kuongeza ufanisi.
“Tunatarajia kufanya maonyesho rasmi Dodoma tutumie nafasi hii kama TASIM tujitangaze kwenye vyombo vya habari ili wafanyabiashara washiriki na kutangaza bidhaa zao na tutangaze kwenye balozi zilizopo hapa nchini ili zione namna ya kusaidia wajasiriamali,” alisema
Alisema viwanda vidogo vidogo vimekuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa Tanzania kwa kuchangia kutoa ajira nyingi na kupunguza kiwango cha umaskini.
Dk. Simbachawene alisema viwanda vidogo ni injini ya ukuaji wa uchumi kwa kuzalisha bidhaa na huduma muhimu na kukuza ujasiriamali wa ndani kwa watanzania walio wengi ambao wako kwenye sekta isiyo rasmi.
Mwenyekiti wa TASSIM, Masoud Ali alisema lengo la kuanzishwa kwa chama hicho ni kuinua viwanda vidogo vidogo ambavyo ndivyo uti wa mgongo wa uchumi wan chi na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kwenye sekta ya viwanda.
Alisema ikakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 99 ya viwanda vyote nchini viko kwenye makundi ya viwanda vidogo sana, viwanda vidogo sana na viwanda vya kati kwa maana ya small, micro and medium industries.
“Kwa hiyo sisi wawakilishi wa haya makundi tuna mchango mkubwa sana kwenye maendeleo ya nchi yetu na kauli mbiu ya TAMISID 2024 ni kusherehekea nguvu ya viwanda vidogo,kujenga Tanzania imara na kuwekeza kwenye mustakabali wetu kwa kuwekezesha watu wetu,” alisema
Alisema kauli mbiu hiyo inaonyesha dhamira ya dhati ya chama hicho kuinua vianda vidogo vidogo na kuvitumia ipasavyo kama injini ya ukuaji wa uchumi na kuomba wadau kujitokeza kuwekeza kwenye sekta ya viwanda.
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo