Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar
KILIO kilichokuwepo nchini kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuingia madarakani, kwamba Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inakimbiza wawekezaji hakipo tena.
Kilio hicho, ndicho uliokuwa wimbo wa vyama vya upinzani, wafanyabiashara na wadau wengine. Ilikuwa ni kawaida kula kukicha, kwenye mitandao ya kijamii zilikuwa zikiandikwa habari za wafanyabiashata nchini kuhamishia biashara zao nchi jirani.
Lakini kwa sasa, kilio hicho hakipo tena, waliokuwa wakilalamika, wametulia kimya? Swali la kujiuliza ni kilipoishia kilio hicho? Jibu lipo wazo, japo watu hawataki kusema ukweli.
Lazima ieleweke wazi kwamba nchi yoyote ikitengeneza mazingira ya biashara yasiyokuwa rafiki, wawekezaji wapya ni lazima wataogopa kuja na waliopo watakuwa hawana uhakika na biashara zao, kwani wanawakuwa hawaelewi kesho yake itakuwaje.
Kama mazingira ya biashara siyo ya rafiki, wawekezaji wapya wanaogopa kuja, bado hata wale waliopo watakuwa wakitamani kuondoka.
Ndiyo maana wataalam wa masuala ya uchumi wanaamini sana kwenye msemo usema uwekezaji ni bidhaa yenye aibu sana, inaona aibu kuwepo mahali ambapo siyo sahihi.
Kwa kutambua falsafa ya biashara Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa mstari wa mbele kuboresha mazingira ya uwekezaji, ambapo kwa sasa nchi inazidi kupata wawekezaji wapya na wale waliopo wakiridhishwa na utulivu wa mazingira ya uwekezaji nchi.
Serikali ya Rais Samia imekuwa mstari wa mbele kuondoa vikwazo vya kibiashara na yale mazuri kwa wawekezaji ikiendelea kuyakumbatia.
Kwa kufanya hivyo tumeshuhudia uchumi wa Tanzania ukiendelea kukua vizuri tangu Rais Samia aliposhika wadhifa huo, Machi, 2021. Kwa ukuaji wa uchumi huo tija inaonekana.
Miongoni kwa taasisi zinazotambua mchango wa Rais Samia katika kukuza uchumi ni Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI), ambapo wiki hii limempongeza Rais Samia kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na wafanyabiashara nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa CTI, Paul Makanza, wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa shirikisho hilo.
Anasema tangu aingie madarakani Rais Samia amekuwa akipambana kuweka mazingira mazuri ya biashara hali ambayo imewavutia wawekezaji wengi kuendelea kuja nchini.
“Ushahidi wa hiki ninachokisema ni takwimu zinazotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) Gilead Teri, kila akitoa takwimu zinaonesha wawekezaji wanazidi kuongezeka hii ni dalili kwamba mazingira yamekuwa mazuri sana,” anasema na kuongeza;
“Tunamshukuru Rais kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara tangu aingie madarakani tunajua bado kuna mengi ya kufanya lakini uelekeo umekuwa mzuri na sisi tumeona tuseme asante kwasababu tunajua kuna mengi mazuri yatafanyika.”
Anasema CTI inashukuru kuona kwamba miundombinu ambayo itawasaidia wafanyabiashara na wenye viwanda kwenye shughuli zao za uzalishaji, kama ujenzi wa bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) na ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR unaendelea vizuri.
“Kinachotukwaza sasa ni umeme, lakini JNHPP ikikamilika suala la umeme litakuwa la uhakika ila tunachoomba ni mradi ukamilike mapema sana na SGR nayo ikikamilika itatusaidia sana kwa sababu mbali na uharaka, lakini ni rahisi sana kuliko kusafirisha kwa barabara,” alisema
Anaiomba Serikali ipunguze gharama za stempu za kielekrtoniki kwani zimekuwa zikiongeza gharama za wenye viwanda na wafanyabiashara na kusababisha bei kuwa kubwa na kuwa mzigo kwa walaji.
Anasema ni vigumu kwa sekta ya viwanda nchini kuwa na ushindani wenye haki wa bidhaa kama kutakuwa na bidhaa bandia zinazoingia kutoka nje ya nchi.
Anasema uchumi hauwezi kukua na kufikia Dira ya Taifa la Maendeleo kama viwanda havitafanya vizuri na kuongeza kuwa kuna haja kwa Serikali kushughulikia vikwazo vyote vinavyowakabili wafanyabiashara na wenye viwanda ikiwemo kudhibiti bidhaa feki.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdalah, analitaka Shirkikisho la Wenye Viwanda (CTI) kushirikiana na taasisi za Serikali kuwafichua wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa bandia kwenye masoko ya Tanzania.
Anasema bidhaa bandia zimekuwa zikisababisha ushindani usiohalali kwenye soko kwani bidhaa hizo zimekuwa zikiuzwa kwa bei rahisi.
“Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ICT yanaweza kusaidia vita dhidi ya bidhaa bandia kuwa rahisi, kwa hiyo wenye viwanda na wafanyabiashara wajikite kwenye matumizi ya ICT,” alisema
Aliipongeza CTI kwa kazi kubwa wanayofanya kuhakikisha inakuwa sauti kubwa ya wenye viwanda nchini.
Naye Mkurugenzi wa Kudhibiti Bidhaa Nchini wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija alisema wananchi wanapaswa kuwa makini kutokana na bidhaa bandia zinazoingia.
Alisema Serikali imekuwa ikidhibiti kwa kiwango kikubwa uingiaji wa bidhaa hizo ingawa wanaoingiza wamekuwa wakibadilisha mbinu mara kwa mara ili kukwepa mkono wa serikali.
“Bidhaa feki zimeongezeka kwenye vipuri vya pikipiki, magari na vifaa vya umeme, hivi vimejaa sana sokoni kwasababu mahitaji ya vipuri hivi yamekuwa makubwa sana,” alisema
Alisema ni wajibu wa kila mmoja wakiwemo wafanyabiashara na wenye viwanda na taasisi za serikali kusaidia kuibua wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa bandia na zisizo na viwango.
Alisema bidhaa bandia na hafifu zimekuwa zikisababisha anguko la bidhaa halisi sokoni kutokana na kuuzwa kwa bei ya chini hali ambayo imekuwa ikiwavutia wateja wengi.
Alisema wazalishaji wa bidhaa wanapaswa kuweka alama ili kuwezesha walaji kutambua kwa urahisi kati ya bidhaa halisi na zile hafifu.
Mbali na changamoto hizo za uwepo wa bidhaa bandia na hafifu sokoni zinazotokana na wafanyabiashara wachache wasio waaminifu, dhamira ya Rais Samia kuzidi kuifungua nchi kibiashara imeendelea kubaki pale pale .
Dhamira hiyo ya Rais ndiyo imechangia kufuta na kupunguza tozo, ada na faini zisizopungua 232 kati ya 380 zilizobainishwa katika utekelezaji wake sawa na asilimia 61.
Hatua hiyo imefikiwa na Serikali kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI).
Akizungumza katika Kikao Maalum cha Kikundi Kazi cha Mazingira ya Biashara jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu wa Bunge, Dkt. Jim James Yonazi, anasema tozo, ada na faini hizo zilikuwa kero kubwa kwa ustawi, ukuaji na maendeleo ya biashara na uwekezaji hapa nchini.
“Maamuzi haya yanaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifungua Tanzania na kuwa kivutio cha kufanya biashara na uwekezaji,” alisema Dkt. Yonazi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi kazi hicho cha Baraza la Taifa la Biashara(TNBC).
Akielezea zaidi mafanikio yaliyopatikana tangu MKUMBI uanze kutekelezwa, Dkt. Yonazi alisema jumla ya Sheria, Kanuni na Taratibu zipatazo 40 kati ya 88 sawa na asilimia 45.5 zimeshapitiwa na kufanyiwa marekebisho.
“Maboresho haya yote ya Sheria, Kanuni na Taratibu yamesaidia kuchochea ukuaji wa sekta za uchumi hapa nchini zikiwemo sekta za uwekezaji, viwanda na biashara, kilimo, mifugo, afya, maliasili na utalii,” anasema.
Dkt. Yonazi anasema Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa TNBC ameelekeza kuendelea kusimamia utekelezaji stahiki wa MKUMBI sambamba na uhamasishaji wa matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa lengo la kuongeza ufanisi kwa wafanyabiashara na wawekezaji hapa nchini.
“Nina agiza Wakurugenzi na Idara za Uratibu, Ufuatiliaji na Tathmini pamoja na Maendeleo ya Sekta Binafsi katika Ofisi ya Waziri Mkuu,wafuatilie utekelezaji wa Maazimio ya TNBC na kuwaandikia barua Makatibu Wakuu wote ambao bado hawajawakilisha taarifa za utekelezaji wa maazimio hayo,” alisisitiza Dkt. Yonazi.
Dkt. Yonazi alimpokeza Katibu Mtendaji wa TNBC Dkt. Godwill Wanga na watendaji pamoja na wafanyakazi wote wa baraza kwa kazi nzuri na kuwakumbusha wajumbe wote kwenye Kikundi Kazi cha Mazingira ya Biashara kuendelea kufanyia kazi maono na matarajio ya Rais Samia.
Kwa upande wake, Dkt. Wanga anasema Kikosi Kazi cha Mazingira ya Biashara kina jukumu kubwa la kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara yanaendelea kuwa rafiki kwa biashara, uwekezaji na uchumi kwa ujumla na kuvutia uwekezaji kujenga uchumi wan chi.
“Kikundi kazi hiki kina jukumu kubwa la kuondoa na kupunguza gharama za kufanya biashara na uwekezaji. Hivi hatuna budi kufanya kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha tunaandaa na kuwakilisha mapendcekezo yenye tija kwa Baraza,” alisema Dkt. Wanga.
Anasema TNBC hufanya kazi kupitia mikutano na vikao katika ngazi mbalimbali kama vile ya Baraza,Kamati Tendaji za Baraza, Mashauriano ya Kiwizara kati ya Sekta Binafsi na Umma(MPPD), Kikosi Kazi cha Kiufundi cha Kiwizara(MTWG), Mikutano ya Baraza la Biashara ngazi ya Mkoa (RBC) na Wilaya (DBC)’
Katibu Mtendaji wa TNBC Dkt. Godwill Wanga, anasema Kikosi Kazi cha Mazingira ya Biashara kina jukumu kubwa la kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara yanaendelea kuwa rafiki kwa biashara, uwekezaji na uchumi kwa ujumla na kuvutia uwekezaji kujenga uchumi wan chi.
“Kikundi kazi hiki kina jukumu kubwa la kuondoa na kupunguza gharama za kufanya biashara na uwekezaji. Hivi hatuna budi kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha tunajiandaa kuwakilisha mapendekezo yenye tija kwa Baraza,” anasema Dkt. Wanga.
Anasema TNBC hufanya kazi kupitia mikutano na vikao katika ngazi mbalimbali kama vile ya Baraza, Kamati Tendaji za Baraza, Mashauriano ya Kiwizara kati ya Sekta Binafsi na Umma (MPPD), Kikosi Kazi cha Kiufundi cha Kiwizara(MTWG), Mikutano ya Baraza la Biashara ngazi ya Mkoa (RBC) na Wilaya (DBC).
Kwa upande wake Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, anapongeza jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia, kukuza uwekezaji nchini.
Kikwete ametoa pongeza hizo juzi jijini Dodoma kwenye Mkutano wa Nne wa Maendeleo ya Biashara na Uchumi uliofanyika katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
“Hayo ndiyo tulikuwa tunasema kama mazingira ni rafiki wale wasiokuwepo wanatamani kuja, lakini mazingira kama sio rafiki wanaogopa kuja na waliopo wanatafuta namna ya kutoka, hawaongezeki zaidi ya pale,” alisema Kikwete na kuongeza;
“Wale wanaokuja wanauliza wamebadilika kweli wale! Ebu ngoja tuone, tupime upepo.” Alisema kwao (kama yeye Kikwete) wanaozunguka duniani, wanaona wawekezaji wanajiamini kuja kuwekeza nchini, wanasema tunapenda kuja kuwekeza Tanzania, tunawaambia njoo.”
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela Judith Ferdinand
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika