Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar
UONGOZI wa Rais Samia Suluhu Hassan, umekuwa na matokeo ya kujivunia katika sekta ya utalii. Hiyo ni kutokana na matokeo mazuri ambayo Tanzania imepata ikiwemo kuongeza idadi kubwa ya watalii wa kimataifa.
Hatua hiyo imeongeza kwa kiasi kikubwa ukuaji uchumi wa Tanzania kulingana na taarifa za utafiti za Barometer ya Utalii ya Dunia ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UNWTO).
Tanzania imeibuka kama moja ya mataifa yanayoongoza kwa utalii, kwa kushika nafasi ya tano duniani sambamba na nchi kama Qatar na Saudi Arabia.
Taarifa hiyo inaonesha mafanikio ya sera za Rais Samia za kufufua sekta ya utalii ndizo zimezaa matunda hayo.
Aidha, Tanzania imeshika nafasi ya nne kwa takwimu za Januari hadi Machi, 2024 katika nchi zilizoongeza mapato yanayotokana na shughuli za utalii duniani na kushika nafasi ya kwanza barani Afrika.
Kwa takwimu za Benki ya Dunia za Mei, 2024, Tanzania imefanikiwa kupata Dola Bilioni 5.75 kutokana na ongezeko la watalii walioingia nchini.
Katika kipindi cha uongozi wake wa Rais Samia tangu aingie madarakani kwa upande wa kuvutia watalii kutoka nje ya nchi, Tanzania imefanikiwa kuongeza watalii kwa zaidi ya asilimia 96, ambapo hadi kufikia Desemba, 2023 watalii wa nje walikuwa takribani milioni 1.8 na watalii wa ndani kiwango kiliongezeka hadi kufikia asilimia asilimia 152, ambapo watalii takribani milioni 1.9 walifika hadi Desemba 2023.
Kutokana na jitihada za Rais Samia, Tanzania imeweza kutambulika kimataifa ambapo kupitia takwimu za Shirika la Utalii Duniani kwa mwaka 2023, Tanzania ilishika nafasi ya 12 duniani kwa kuwa na ongezeko la idadi ya watalii wa kimataifa kabla ya janga la UVIKO 19.
Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2024/2025 imeendelea kuakisi umuhimu wa kuendelea kukuza Uchumi na kuweka mkazo katika kuweka mazingira bora ya uwekezaji na biashara, kukuza ajira, kukamilisha miradi ya maendeleo ya kimkakati na kwamba kati ya Sekta chache zilizopewa kipaumbele , Sekta ya Utalii pia imeonekana.
Katika muda mfupi tu, Rais Samia ameweka kipaumbele kwa utalii kama injini kuu ya ukuaji wa uchumi kwa kuanzisha mipango ya kimkakati ya kuongeza mvuto wa kimataifa wa nchi, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu, kampeni za uhamasishaji ushirikiano na mashirika ya kimataifa ya usafiri.
Juhudi hizi zimesababisha ongezeko la watalii wanaovutiwa na mandhari nzuri ya Tanzania, wanyamapori wake wa aina mbalimbali, na urithi wake.
Kuongezeka kwa utalii pia kunachangia mapato kwa Taifa na uzalishaji wa ajira kwa Watanzania, hususan katika maeneo ya vijijini, ambako fursa za kiuchumi mara nyingi ni chache.
Hii inaendana na dhamira ya Rais Samia ya kuhakikisha maendeleo ya uchumi jumuishi, ambapo faida za utalii zinawafikia wananchi wote.
Zaidi ya hayo, msisitizo wa Rais Samia kwenye utalii endelevu unaiweka Tanzania mbele kama kivutio kinachowajibika.
Kwa kukuza miradi rafiki kwa mazingira, serikali yake inalinda uzuri wa asili wa nchi wakati huo huo ikivutia watalii wanaojali mazingira. Mbinu hii haihifadhi tu mifumo ya kipekee ya mazingira ya Tanzania, bali pia inaimarisha ustahimilivu wa sekta ya utalii dhidi ya changamoto za siku zijazo.
Tanzania inavyozidi kupanda kwenye ramani ya utalii wa kimataifa, kwa msaada wa mashirika ya kimataifa kama UNWTO, uongozi wa Rais Samia unathibitisha kuwa maono wazi na hatua za kimkakati zinaweza kusababisha mabadiliko makubwa ya kiuchumi.
Yote hayo yanatokana na maono makubwa na falsafa za Rais Dkt. Samia, kwenye Sekta ya Utalii nchini yameendelea kuleta mafanikio mengi kwenye anga za Kitaifa na Kimataifa kila siku.
Maono hayo yameifanya Tanzania kuendelea kung’ara na kuwa ndiyo nchi inayoongoza kwa kuwa kivutio cha watalii barani Afrika kwa mwaka 2024.
Aidha, dunia imeendelea kushuhudia kwa mara nyingine Serikali inayoongozwa na Rais Samia, imevunja rekodi na kuandika historia ya kipekee duniani kwa vivutio vyake viwili kushinda tuzo kubwa za utalii barani Afrika tena kwa mara sita kila mmoja mwaka huu 2024!
Hiyo inatokana na Serikali ya Tanzania kupewa tuzo nne na taasisi maarufu duniani kwa utoaji wa tuzo za sekta ya utalii, Taasisi ya Tuzo za Dunia za Utalii Kanda ya Afrika (World Travel Awards Africa – Gala) kwenye usiku wa tuzo uliofanyika kwenye jiji la Mombasa nchini Kenya, mwaka huu ambapo Tuzo ya kwanza ikiwa ni hiyo ya kuwa “nchi inayoongoza kuwavutia watalii barani Afrika kwa mwaka 2024.”
Tuzo nyingine ilikwenda kwa Bodi ya Utalii ya Tanzania ambapo ilipewa tuzo ya kuwa Bodi Bora inayoongoza Barani Afrika kwa mwaka 2024.
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia eneo la utalii, Nkoba Mabula ndiye aliyeiongoza ujumbe wa Serikali ya Tanzania Mombasa, nchini Kenya kupokea tuzo hizo.
Zanzibar nayo imetangazwa kuwa eneo maridhawa kwa Matukio na Matamasha (African’s Leading Festivals and Events Desnation 2024), na wadau wengine kama hoteli ya Kifahari ya Thanda iliyojengwa kwenye Kisiwa cha Shungimbili huko Mafia ikiendelea kushinda mara sita katika tuzo ya kundi la hotel ya kifahari iliyopo kwenye Kisiwa barani Afrika 2024 yaani African’s leading luxury Island 2024.
Tuzo ya tatu na ya nne kwa Serikali zilikwenda kwa Hifadhi za Serengeti na Mlima Kilimanjaro ambapo Mlima Kilimanjaro umeshinda tuzo hii ya Kivutio Bora barani Afrika mara sita kuanzia mwaka 2013, 2015, 2016, 2017, 2018 na 2024 wakati Hifadhi ya Serengeti nayo ikishinda mara sita mfululizo kuanzia mwaka 2019.
Kwa tuzo hizo, Tanzania imeweza kuandika historia ya Sita Kubwa za Sekta ya utalii kwa mwaka 2024.
Akikabidhi tuzo hizo, Mwanzilishi wa Taasisi ya World Travel Awards Africa- Gala, Graham Cooke, alisema taasisi yake imetangaza hifadhi mbili za Tanzania (Serengeti na Mlima Kilimanjaro) kuwa washindi kwenye kipengele cha Hifadhi na Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika kwa mwaka 2024.
Hifadhi ya Taifa Serengeti imetangazwa kuwa mshindi katika kipengele cha Hifadhi Bora barani Afrika (Africa’s Leading National Park 2024) wakati Mlima Kilimanjaro ikitangazwa Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika (African Leading Tourism Attraction 2024)
Hifadhi ya Serengeti imezishinda hifadhi nyingine kwa ubora barani Afrika ilizoshindanishwa nazo ambazo ni Maasai Mara ya nchini Kenya, Kruger ya Afrika Kusini, Central Kalahari ya Botswana, Etosha ya Namibia na Kidepo Valley ya nchini Uganda.
Mlima Kilimanjaro umevishinda vivutio vingine vya utalii ambavyo ni Hifadhi ya Ngorongoro, Hartbeespoort aerial Cableway, V&A, Waterfront, Robben Island, Table Mountain zote za Afrika Kusini. Pia Ziwa Malawi, Okavango Delta ya Botswana, na Pyramid of Giza ya Misri.
Hivi karibuni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana, akiwa kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Hifadhi ya Mikumi na Ruaha pia wakati wa kukabidhi kikosi maalum cha wapiganaji wa Jeshi la JWTZ kupandisha Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro alimshukuru Rais Dkt. Samia, kwa kuendelea kuitangaza Sekta ya Utalii duniani kupitia Filamu ya Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania.
Alitoa wito kwa Watanzania kuunga mkono jitihada za Serikali za kutangaza utalii kwa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Kutangaza Tanzania iliyoratibu Filamu ya Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania amefafanua kuwa Wizara itaendelea kusimamia kikamilifu Sera ya Utalii na kutangaza vivutio vya utalii kimkakati duniani ili sekta iweze kuchangia kwenye uchumi wa Tanzania.
Hivi sasa Sekta ya Utalii inachangia takribani asilimia 17 kwenye pato la Taifa na takribani asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni, ambapo kutokana na kuimarika kwa vivutio vya utalii idadi ya watalii kutoka nje imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,808,205 mwaka 2023 sawa na ongezeko la takribani asilimia 95.
Aidha, mapato yameongezeka kutoka dola za Kimarekani milioni 1,254.4 kwa mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Kimarekani Milioni 3,373.83 mwaka 2023.
Hii ina maana kuwa Tanzania imevunja rekodi ya kufikia Idadi ya juu zaidi ya watalii kuwahi kufikiwa, lakini pia kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii(UNWTO) kwa ongezeko hilo, Tanzania imekuwa nchi ya pili Afrika baada ya Ethiopia na ya 11 duniani miongoni mwa nchi zilizoongeza watalii wengi baada ya Uviko -19 hasa ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2019 kabla ya Uviko -19.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Rais Samia, anataka kuona utalii unazidi kuiongezea Tanzania mapato. Kwa kutmbua hilo, ameahidi kufanya filamu nyingine ya Royal Tour katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi baada ya kujionea wanyamapori mbalimbali katika Hifadhi hiyo.
Dkt. Samia, ametoa ahadi hiyo kufuatia ombi la Waziri Mkuu Mstaafu, Mzengo Pinda, baada ya kutembelea hifadhi hiyo ya Katavi.
Rais Samia, anasema tayari Serikali yake imeshaona mambo mengi ya kufanya mle ndani, nakuongeza kuwa suala la kuandaa filamu nyingine ya ‘Royal Tour,’ kuitangaza Hifadhi hiyo limeshafanyiwa kazi na Waziri wa Maliasili na Utalii na taratibu zikishakamilika ataenda mwenyewe kwa kazi hiyo.
“Nataka nikiri kwamba zile sifa alizozisema Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee Pinda, kuhusu uwepo wa wanyama wengi na wa kuvutia katika Hifadhi ya Katavi na mambo mengine nimeziona mwenyewe, maana nilipita kwenye mbuga hiyo kuona ikoje mahitaji yakoje,” anasema Mhe. Samia.
Hifadhi ya Taifa ya Katavi inapatikana mkoani Katavi ikiwa ndani ya wilaya tatu za mkoa huo. Wilaya hizo ni Mlele, katika Halmashauri ya Mpimbwe, Wilaya ya Tanganyika na Wilaya ya Mpanda katika Halmashauri ya Nsimbo.
Mojawapo ya kivutio kinachopatikana kwenye Hifadhi ya Taifa ya Katavi ni, Mto Ndido wenye maji meupe, ambapo utalii wa kuvua samaki (Spot Fishing) huvutia watalii wengi kutokana mto huo kuwa wenye maji yanayoonesha samaki aina ya kambale na kamongo wanaozaliana kwa wingi.
Aidha mto huo una mawe ya kuvutia yenye maumbo mduara mithili ya golori ndani ya maji kuna wadudu wa aina mbalimbali.
Maji ya Ziwa Katavi yakiwa mengi baadhi ya samaki husafiri na kwenda kwenye mito mingine iliyopo nje ya hifadhi ambao wanaweza kuvuliwa na wananchi wa maeneo hayo kwa vibali maalumu vya Serikali.
Ukiachilia mbali utalii wa kutazama wanyama mbalimbali wenye maumbo makubwa wakiwa kwenye makundi makubwa ndani ya hifadhi hiyo, pia kivutio kingine ni Ziwa Katavi ambalo lipo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi, ni idadi kubwa ya viboko kuliko hifadhi zote zilizopo nchini.
Aidha, Hifadhi ya Taifa ya Katavi, ina Simba wanaotembea kwa makundi, Twiga, Swala, Tembo, Chui, Pundamilia, na aina mbalimbali za ndege.
Pia, ndani ya hifadhi hiyo, lipo zao la utalii wa utamaduni ambapo unahusisha makabila mawili; Wabende na Wapimbwe ambao wana tamaduni za kuabudu mizimu ambao ndio asili ya jina la Mkoa wa Katavi.
Mkoa wa Katavi umetokana na mwindaji aliyeitwa Katavi, huyu alikuwa kiongozi wa kimila aliyeshughulikia masuala ya matambiko ya Wapimbwe na Wabende.
Kabla ya kuwa na hifadhi wawindaji waliamini kuwa kabla ya kwenda kuwinda ni lazima wapite kwenye mti wa Mkwaju uliotumiwa na Katavi kama eneo la matambiko.
Hifadhi ya Taifa ya Katavi ilianzishwa mwaka 1974, kati ya hifadhi 21 zilizopo nchini na inashika nafasi ya tano kwa ukubwa, ambapo ina jimla ya kilometa za mraba 4,471.
Takwimu kutoka sekta ya utalii zinaonesha kuwa hadi kufikia Agosti, 2024 Tanzania imepokea idadi ya watalii wa kimataifa 2,026,378 ikiwa ni kiwango cha juu kabisa kuwahi kufikiwa kwenye historia ya Tanzania na mapato yatokanayo na sekta hiyo, kufikia Dola za Marekani bilioni 3.5.
Sekta ya Utalii imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania, huku ikichangia asilimia 17.2 ya Pato Ghafi la Taifa, asilimia 25 ya mauzo ya nje na kuzalisha ajira zaidi ya milioni 1.5 ikiwa ni ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kupitia mnyororo wake wa thamani.
More Stories
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia
Mwitikio watoto kushiriki vita dhidi ya mabadiliko tabianchi