March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maonesho ya Nanenane Kanda ya Magharibi kufanyika Tabora

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online -Tabora

TAASISI mbalimbali, wadau wa maendeleo na wakazi wa Mikoa ya Tabora, Kigoma na Mikoa jirani wamehimizwa kujitokeza kwa wingi katika maonesho ya wakulima Nane Nane Kanda ya Magharibi ambayo yanatarajiwa kuanza Agosti 1-8 mkoani Tabora.

Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora,Dkt. John Mboya,wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake ambapo alibainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yamesheheni mambo mengi mazuri.

Amesema kuwa maonesho hayo ya sikukuu ya wakulima hufanyika kila mwaka nchini na kwa Kanda ya Magharibi yanafanyika katika Viwanja vya Nane Nane Ipuli Mjini Tabora na kushirikisha Mikoa miwili ya Tabora na Katavi.

Dkt. Mboya amesema maonesho hayo kwa mwaka huu yana kauli mbiu isemayo ‘Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi: Viongozi Bora ndiyo msingi wa maendeleo.

Ametaja taasisi zilizoshiriki maonesho ya mwaka jana kuwa ni za sekta ya umma, binafsi, halmashauri za Mkoa wa Tabora na Kigoma, taasisi za serikali, majeshi, utafiti, kampuni za simu, taasisi zisizo za serikali na tasisi za fedha.

‘Natoa wito kwa wakazi wote wa Mikoa ya Tabora na Kigoma na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho haya ili kunufaika na fursa lukuki zilizopo ikiwemo kujipatia bidhaa bora za wakulima na wajasiriamali, ameeleza.

Dk Mboya amedokeza kuwa waliohudhuria maonesho ya mwaka jana walipata manufaa mengi, ikiwemo elimu, teknolojia za kilimo na ufugaji, fursa za masoko na kuongeza mnyororo wa thamani kwa bidhaa za mazao, mifugo na uvuvi.

Amesisitiza kuwa maonesho hayo ni fursa muhimu kwa taasisi, wakulima, wafanyabiashara na wadau mbalimbali kuonesha bidhaa wanazozalisha na kuziuza, kuonesha uwezo wao wa kuendeleza sekta ya kilimo.

Aidha kupitia vipindi wakulima na wadau wote wataweza kujua na kujifunza teknolijia bora za uzalishaji bidhaa zilizopo hapa nchini, pia watapata taarifa kuhusu sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

RAS ameongeza kuwa Viongozi wa kitaifa watakaoshiriki maonesho hayo kama wageni rasmi watapata wasaa wa kutoa maagizo na maelekezo yenye tija kwa wananchi.

.