October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania kuanza Dar kesho

Na Angella Mazulla, TimesMajira, Online Dar

WIZARA ya Viwanda na Biashara kupitia taasisi yake ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade),imewaomba Watanzania kutembelea Maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yanayotarajia kuanza leo na kumalizika Desemba 9,2020.

Akizungumza leo jijini Daer es Salaam Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis amesema uanzishwaji wa maonesho hayo ulilenga kuhakikisha ujenzi wa uchumi wa viwanda unakuwa na matokeo chanya katika uchumi.

Amesema maonesho haya yanalenga kuwezesha wadau wa Sekta ya Viwanda kupata fursa ya kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kutangaza fursa zilizopo katika sekta hiyo.

“Maonesho hayo yanalenga kutoa fursa ya kuvitambua viwanda vya Tanzania pamoja na bidhaa zinazozalishwa nchini ili Watanzania wazitambue na kupenda kuzitumia ,kuhamasisha Watanzania kutumia bidhaa na huduma zinazozalishwa hapa nchini,”alisema.

“Pia yanalenga kuwaunganisha wenye viwanda na wazalishaji mbalimbali wa malighafi na huduma zingine zinazotumika viwandani na kuwaunganisha wenye viwanda na wasambazaji wa teknolojia za viwanda,”amesema

Khamis amesema kauli Mbiu ya Maonesho hayo ni; “Tumia Bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania.”

Amesema lengo la kauli mbiu hiyo ni kuhamasisha Watanzania waendelee kupenda, kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya Tanzania kwa lengo la kuchochea uzalishaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi ili kukuza soko la ndani na hatimaye kuiwezesha Tanzania ambayo imeingia katika Uchumi wa Kati.