November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maonesho ya biashara kukutanisha wafanyabiasha zaidi ya 1,000 kesho

Na Daud Magesa, TimesMajira, Online Mwanza

WAFANYABIASHARA na wadau zaidi ya 1,000 wa sekta ya utalii Tanzania na nje ya nchi wanakutana jijini Mwanza katika Jukwaa la Biashara (Tanzania Business Summit) kufanya maonesho ya biashara, utalii na uwekezaji.

Mratibu wa Jukwaa hilo, Bernad Mwata amesema juzi maonesho yatafanyika Rock City Mall kwa siku tatu kuanzia Aprili 30 hadi Mei 2, mwaka huu, yakishirikisha wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Kenya, Burudi, Uganda, Rwanda na Afrika ya Kusini.

Amesema maonyesho hayo yanalenga kuwakakutanisha wafanyabiashara ili kupata uelewa wa masoko, kujitangaza na kuleta fursa za kibiashara na kiuchumi na kuwataka wafanyabiasha wa jiji la Mwanza kushiriki ili kupata uelewa wa masoko ya bidhaa zao,mbinu za biashara,uwekezaji,kujitangaza na kuchangamkia fursa za biashara.

Naye Mkurugenzi wa Kiwanda cha Mafuta ya Alizeti cha Nyahita Sunflower Coocking Oil na taasisi ya mikopo ya Zanziba & Nyahita Microfinance,Nyahita Nyahita amesema ni fursa kubwa na yenye manufaa makubwa kwa wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo wa utalii nchini.

Amesema maonesho hayo yanakwenda sambamba na maono ya Tanzania ya viwanda kuelekea uchumi wa kati yaliyohamasishwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati John Magufuli, ambapo binafsi yalimsukuma kuanzisha kiwanda cha kusindika mafuta ya Alizeti na amewahamasisha wakulima wilayani Rorya kulima zao hilo.

Nyahita amempongeza Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuonesha upeo mkubwa wa uongozi na kuwatia moyo wafanyabiashara nchini hali ambayo itawawezesha kufanya biashara zenye tija kwa weledi ili kukuza uchumi na pato la taifa.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kusindika Mafuta ya Alizeti, Nyahita Sunflower Coocking Oil, Nyahita Nyahita akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa maonyesho ya biashara, utalii na uwekezaji (Tanzania Business Summit) yatakayofanyika kwa siku tangu kuanzia Aprili 30 hadi Mei 2, mwaka huu jijini Mwanza.Picha na Daud Magesa

Amesema kupitia kampuni yake ya Zanziba & Nyahita Microfinance , inawashika watu wa hali ya chini kwa kuwatengeneza waonekane nyota kwa urahisi, kuwaelimisha kuhusu fursa, kuwakopesha ili waweze kukua na kupiga hatua ya maendeleo.

Aidha ametoa wito kwa wafanyabiashara kujitokeza kwenye maonesho hayo ili kupata elimu ya biashara,fedha, mitaji, masoko, teknolojia ya viwanda na mashine ili kuboresha bidhaa zao na hatimaye kutengeneza ajira, kuongeza mapato yao na ya serikali (kodi).

“Maonesho hayo yataipa Serikali fursa ya kuifikia jamii, kutengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji na Watanzania kufanya biashara yenye tija na kuzalisha ajira na kutolea mfano Zanziba & Nyahita Microfinance tangu 2019 imewekeza sh. bilioni 3 za mikopo na imewanufaisha wajasirimali 10,000 (akina mama, vijana na wanaume),”amesema Nyahita.

Amefafanua kuwa taasisi hiyo inalenga kumjenga Mtanzania asiishi maisha tegemezi bali kuona kesho yake inakuwa njema.

Naye Meneja Masoko wa kampuni ya Chroride Exide (T) Ltd ambao ni wadhamini wakuu wa maonesho ya Tanzania Business Summit, Geogete Irumba amesema wafanyabiashara watapata fursa nzuri ya kujitangaza pia kutoa elimu kwa watumiaji wa bidhaa zao hasa zinazokwenda kwa teknolojia ya kisasa.

“Kampuni ya Chloride Exide Tanzania inayojishughulisha na uuzaji mifumo ya nishati ya jua, betri za magari na mfumo wa umeme wa ziada, mbali na kujitangaza kupitia maonyesho hayo tutatoa mafunzo (elimu) kwa watumiaji wa bidhaa zetu,”amesema.