Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Maonesho ya Biashara Arusha yanayojulikana kama Arusha Trade Fair ni maonesho makubwa ya kibiashara ya mwishoni mwa mwaka inayotarajiwa kufanyika kuanzia Jumatatu ya tarehe 13 hadi Jumapili ya terehe 19 mwezi Disemba 2021 katika viwanja vya michezo vya kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha, kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 12 jioni.
Maonesho haya yanayohusisha biashara mbalimbali yanalenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara wakubwa, wa-kati na wafanyabiashara wadogo (wajasiriamali) kujitangaza na kufanya biashara hasa katika kipindi cha msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Malengo mengine ya Maonesho haya ni kuwa sehemu moja ambapo wananchi wanaweza kujipatia mahitaji yao yote muhimu kimanunuzi wakati wa msimu huu wa sherehe za mwisho wa mwaka.
Ni matarajio kuwa uwepo wa bidhaa anuai kutoka kwa washiriki kutatoa nafasi hii muhimu kwa wanunuzi kupata bidhaa zote sehemu moja.
Kufanyika kwa maonesho haya kwa wiki nzima kunalenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara kuwa na muda wa kutosha wa kufanya biashara na vilevile kwa watembeleaji kuwa na muda mrefu zaidi kufanya manunuzi.
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid pia umechaguliwa kutumika kwa sababu ya umaarufu wake, eneo uliopo na urahisi wa kufikika kwake ambapo hata wageni kutoka nje ya Jiji la Arusha wanaweza kuufikia kwa urahisi.
Maonesho haya yamepangiliwa kwa mfumo wa “Mitaa” ambapo bidhaa zinazofanana hukaa eneo moja linaloitwa ‘mtaa’ na kumrahisishia mtembeleaji kujua aina za bidhaa na wapi kwa kuzipata kirahisi.
Mitaa hiyo ni Pamoja na Mtaa wa X-mas na Mwaka Mpya, Mtaa wa Shule, Mtaa wa Sola na Taa, Mtaa wa Fedha, Mtaa wa Mawasiliano na Mtaa wa Ujasiri Ni Mali.
Ushiriki wa maonesho haya unafanyika kwa njia rahisi ambapo wafanyabiashara wanafanya usajili moja kwa moja kupitia tovuti ya maonesho ya www.arushaholidayfair.com
Maonesho haya yanatarajiwa kukusanya biashara zaidi ya mia moja na watembeleaji wanaotarajiwa kufikia angalau elfu kumi kwa siku zote za maonesho.
Kwa mwaka huu wa 2021, Kampuni ya Mawasiliano ya TIGO ndio Mdhamini Mkuu wa Arusha Trade Fair. Washirika wengine ni pamoja na Access Image, Radar Security, Sun King, Hanspaul, Brandful Media, KnK Grandmaster Records na Clouds Media Group.
Arusha Trade Fair imeandaliwa na kuratibiwa na Bulb Africa, kampuni yenye makao makuu yake jijini Arusha inayojishughulisha na ukuzaji na uendelezaji wa biashara.
“Tigo Tanzania inayo furaha kuwa mdhamini mkuu wa maonesho makubwa ya biashara Arusha 2021, katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid,yanayojulikana kama Arusha Trade Fair 2021.Maonesho haya yanayohusisha biashara mbalimbali yanalenga kutoa fursa kwa wafanyabishara wakubwa,wa-kati na wadogo kujitangaza na kufanya biashara.” Alisema Meneja wa Kanda ya Kaskazini, Daniel Mainoya.
“Kampuni ya Tigo imekuwa mstari wa mbele katika kubuni bidhaa na huduma zinazo walenga wafanyabiashara moja kwa moja kupitia huduma yetu ya Lipa Kwa Simu, tumedhamiria kuhakikisha kila mfanyabiashara atakae kuwa na banda hapa katika maonesho anatumia huduma ya Lipa Kwa Simu. Lipa kwa Simu ni huduma ya kifedha ya kidijitali inayomfanya mfanyabiashara au taasisi kupokea fedha kutoka kwa wateja wanaotumia simu za mkononi.” Aliongezea Mainoya
Gharama za viingilio katika maonesho haya ni Shs. 1,000/- kwa kulipia kupitia huduma ya Lipa Kwa Simu ya tiGO ama Tshs. 2,000/- kwa kulipia kwa pesa taslim mlangoni.
Wito unatolewa kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani kushiriki na kutembelea maonesho hili ili kujipatia bidhaa na huduma mbalimbali kipindi hiki cha msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa