-Wadau Songwe wataka yadhibitiwe ili watu wavuje jasho kujenga nchi.
Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe
WADAU wa maendeleo Mkoa wa Songwe wamebainisha mambo kadhaa ambayo wamesema kuwa yalikuwa kikwazo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendelelo ambayo ukomo wake unafikia mwaka wa 2025 na kutaka yafanyiwe kazi ili kufikia malengo kuelekea dira mpya ya 2050.
Wameyataja mambo hayo kuwa, wananchi kupewa matarajio yasiyokuwa na uhalisia pindi wanapoenda kupata huduma za kiroho ambapo baadhi ya viongozi wa dini huwaaminisha kuwa wanaweza kupata mali au mafanikio pasipo kufanya kazi kwa kuwaombea kuwa daka gari,daka nyumba.
Wametoa maoni hayo, Julai 31,2024 katika kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Daniel Chongolo, kwa lengo la kupokea maoni ya wakazi mkoani humo.
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho, Frida Wikesi, ambaye ni Kamanda wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Songwe, ameeleza kuwa kitendo hicho cha baadhi ya viongozi wa dini kutoa huduma ya maombi kwa kuwaaminisha wananchi kupata mali, utajiri au mafanikio bila kufanya kazi ni miongoni mwa changamoto ambazo zilikwamisha utekelezaji wa dira ya Taifa ya maendeleo ambayo inafikia ukomo wake mwaka 2025.
Wikesi ameshauri changamoto hiyo kufanyiwa kazi kwa viongozi hao kutoruhusiwa kufanya maombi hayo yanayohamasisha watu kupata mali pasipo kufanya kazi na badala yake watumie majukwaa hayo kuhamasisha watu kufanya kazi kwa kuwa kila mtu akifanya kazi kwa bidii taifa lipata maendeleo na Dira ya Taifa ya maendeleo itakuwa imetekelezwa ipasavyo.
Pia alitaja changamoto nyingine iliyokwamisha utekelezaji wa dira ya Taifa ya maendeleo ya 2025 ni kukosekana kwa suala la uadilifu miongoni mwa watu waliopewa dhamana katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Hali hii ya kukosekana kwa uadilifu kumesabisha Taifa kutumia gharama kubwa kukamilisha miradi ambayo imeshindwa kukamilika baada ya ufisadi kufanyika,”amebainisha Wikesi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe, Radwell Mwampashe, ameainisha mafanikio yaliyotokana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendelelo ya 2025 ni suala la utawala bora na hali ya utulivu na amani kwa Taifa.
Pamoja na mambo mengine, washiriki hao walisisitiza na kushauri mikakati inayofaa kwa ajili ya Dira ya Maendelelo ya 2050, huku suala la elimu hasa elimu ya ufundi ili kuendanda na kasi ya ukuwaji wa maendeleo ya dunia.
Kadhalika, wajumbe hao walishauri Taifa kujikita kwenye mipango ya ukuzaji wa teknolojia ya kisasa ili kudhibiti upotevu wa rasilimali, ikiwemo taifa kufanya mapinduzi katika matumizi ya fedha kwa njia za kiteknolojia badala ya watu kutembea na kiasi mikononi kwani hali hiyo itasaidia kupunguza vitendo vya ufisadi na kukuza pato la taifa hatimaye kupunguza utegemezi.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria