Ashura Jumapili, Timesmajira Online,
Bukoba
Shauri namba 17740 la mwaka 2024 la mauaji ya mtoto Noela Asimwe Novart (2.5), aliyekuwa na ualbinolinalowakabiri washitakiwa tisa,Agosti 23,2024 limetajwa tena mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, ambapo upande wa Jamhuri umewasilisha maombi sita na kupokelewa na Mahakama.
Wakili wa Serikali Erick Mabagala akisoma maombi hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,Elipokea Yona,amesema Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba imepokea maombi sita ya kesi ya mauaji ya mtoto Asimwe Novart ili iweze kusikiliza shauri hilo.
Mabagala amesema kuwa maombi hayo yalipelekwa Agosti 21 mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba .
“Tumeamua kupeleka shauri la mauaji lenye namba 17740, liweze kusikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, kwani Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo,”amesema Mabagala
Baada ya kupokelewa kwa maombi hayo ilitolewa amri ya utekelezaji,ikiwa ni kuruhusu shauri kusikilizwa ila taarifa za mashahidi wa kesi hiyo zisitolewe kwa umma, kwa maana ya kutotoa taarifa za mashahidi bila idhini ya Mahakama.
Pia anwani za makazi ya mashahidi kutochapishwa kwa umma,baadhi ya mashahidi kufichwa wakati wakitoa ushahidi,vinasa sauti wakati wa kusikilizwa kwa kesi havitaruhusiwa.
Ameongeza kuwa kutokana na maelekezo hayo ya Mahakama Kuu,aliomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi kuwapangia tarehe ya kutaja kesi hiyo ili maelekezo yaliyotolewa yafanyiwe kazi.
Hakimu Yona alilikubali ombi hilo na kusema kuwa Septemba 6 mwaka huu kesi hiyo ndipo itakapo tajwa tena.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini