Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora
IDARA ya ujenzi Halmashauri ya Manispaa ya Tabora imeingia katika kashfa baada ya baadhi ya Maofisa wake kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ambvyo vimesababisha Manispaa hiyo kupoteza mapato.
Tuhuma hizo zimetolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora,Ramadhan Kapela kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili rasimu ya bajeti ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).
Kapela,ameeleza kuwa idara hiyo inatuhumiwa kutafuna fedha za mapato yatokanayo na utoaji vibali vya ujenzi kutoka kwa wafanyabiashara na wamiliki wa majengo, hivyo kusababisha upotevu wa mapato.
Amebainisha kuwa Manispaa hiyo ilitarajiwa kuingiza zaidi ya milioni 29 za vibali vya ujenzi wa maghala yaliyojengwa katika maeneo mbalimbali ndani ya manispaa hiyo, lakini kiasi kilichowasilishwa ni milioni 2 tu.
Pia Kapela, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Elias Kayandabila,kwa kushirikiana na vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina wa tuhuma hizo na wote watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Kapela amebainisha kuwa hayupo tayari kuona mapato yanaingia kwenye mifuko ya watu binafsi, badala ya kufanya kazi za maendeleo ya wananchi, wahusika wote ni lazima wawajibike.
‘Katika hili nipo tayari kujiudhuru endapo Kiongozi yeyote wa ngazi za juu ataingiza mkono wake, na kutaka kuwalinda hawa wahujumu uchumi wa Manispaa yetu,”.
Amesisitiza kuwa,anachotaka ni haki itendeke kwa kuwa watuhumiwa wamekuwa wakifanya hivyo kwa makusudi bila woga huku wakijua fika kuwa ni kinyume na sheria.
Diwani wa Kata ya Itonjanda Alfonsi Shushi,ameeleza kuwa wamechukizwa na suala hilo na wanamuunga mkono Mstahiki Meya, uchunguzi wa kina ufanyike na Ofisa yeyote atakayebainika afikishwe mahakamani kwa uhujumu wa uchumi.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Tabora Daniel Mhina,amekemea tabia hiyo na kuonya wafanyabiashara na wawekezaji wanaokwepa kulipa kodi na kuiibia syerikali kupitia njia za panya ikiwemo kuwahonga watumishi wa Serikali .
“Inasikitisha kuona Maofisa walioaminiwa na Serikali na kupewa ajira, wakijiingiza katika tuhuma za kula rushwa na kuikosesha mapato halmashauri huku wakijineemesha binafsi, jambo hili halikubaliki,” amesema na kuongeza:
“Siku u chache zilizopita,kulikuwa na malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara wakiwatuhumu baadhi ya watumishi wa Manispaa hii,kwa kuwaomba rushwa ili waruhusiwe kujenga vibanda kwenye stendi ya daladala iliyoko eneo la maduka 30,”.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Elias Kayandabila ,alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo amesema kuwa yuko likizo ila amepata taarifa hiyo na kubainisha kuwa yuko makini na yeye ndiye amekuwa akiibua wanaohujumu mapato ya Manispaa hiyo.
More Stories
Hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wanaohatarisha usalama Mbeya
Mbeya yapokea bil.23.4 ujenzi sekta ya elimu
Shirikisho la Waandishi wa habari Afrika Mashariki laanzishwa kutetea haki za wanahabari